SERIKALI IMEAMUA KWA DHATI KUWEKEZA KWENYE MIRADI YA NISHATI



📌 Mkandarasi Mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) alipwa kwa asilimia 88.7

📌 Mradi wafikia asilimia 95.8


Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kwa dhati kuwekeza katika miradi ya nishati nchini huku lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa upatikanaji umeme nchini unakuwa mkubwa kuliko mahitaji ya nchi.

Amesema hayo tarehe 18 Januari 2024 jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ilipowasilisha taarifa kuhusu hali ya uzalishaji na usambazaji umeme nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.


Kikao ambacho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Katibu Mkuu, Mhandisi, Felchesmi Mramba, baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na Watendaji wa Wizara ya Nishati.

“Moja ya vipaumbele vikubwa vya Serikali ni Sekta hii ya Nishati na ndio maana fedha zimekuwa zikitolewa za kutekeleza miradi mbalimbali ya Nishati ikiwemo mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao gharama yake ni shilingi Trilioni 6.5 na mpaka sasa Serikali imeshamlipa mkandarasi shilingi Trilioni 5.7 ambayo ni sawa na asilimia 88.7.” Amesema Dkt.Biteko

Kuhusu usimamizi wa mradi wa JNHPP amesema kuwa, Serikali iko makini katika usimamizi wake na kwamba kuna mamlaka mbalimbali zinazosimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa ufanisi akitolea mfano Timu Maalum ya Wataalam iliyoundwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusimamia mradi huo ambayo inaongozwa na Profesa Idris Kikula.

Kuhusu hali ya miundombinu ya umeme nchini, Dkt. Biteko amesema kuwa, itaendelea kufanyiwa matengenezo ili iweze kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme kwa ukamilifu wake, huku juhudi za kujenga miundombinu mingine mipya ikiendelea.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alieleza Kamati kuwa, mradi wa umeme wa JNHPP kwa sasa umefikia asilimia 95.8 na kwamba mtambo namba Tisa utakaozalisha megawati 235 umeshakamilika na mtambo Namba 8 na namba 7 iko mbioni kukamilika.

Kuhusu hali ya umeme nchini, Mhandisi Nyamo-Hanga amesema kuwa, pamoja na jitihada mbalimbali zinazoedelea kufanywa na Serikali ili kupunguza changamoto ya umeme nchini, hali ya upungufu wa umeme itaisha mara baada ya kuwashwa kwa kwa mashine mbili za JNHPP zenye uwezo wa megawati 470 ambazo zinatarajiwa kuwashwa kabla ya mwezi Machi, 2024.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dkt. David Mathayo David pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo wamepongeza viongozi wa Wizara ya Nishati kwa usimamizi mzuri wa Sekta na kueleza kuwa wana imani kwamba viongozi hao kwa kushirikiana na Taasisi zake wataiwezasha nchi kuwa na Nishati ya kutosha, ya uhakika na inayotabirika.

Comments