DKT. BITEKO ASHIRIKI ROMBO MARATHON; APONGEZA UBUNIFU WAKE






Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo ameshiriki mashindano ya Rombo Marathon yaliyohusisha mbio za Kilometa tano, kumi na 21 na kupongeza waandaaji kwa ubunifu wao uliopelekea marathon hiyo kuendelea kuimarika kila mwaka ambapo licha ya kulenga katika kuimarisha afya kwa washiriki, imejikita katika kuchangia uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii na utunzaji wa mazingira.


Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo tarehe 23 Desemba, 2023 wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, akiwa ni mgeni rasmi katika  marathon hiyo  ambapo alikimbia kwa umbali wa kilometa Tano akiambatana viongozi mbalimbali wa Kitaifa, Mkoa na Wilaya.


"Nimeelezwa kwamba lengo la Rombo Marathon  ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira, kukuza utalii wa ndani, kuchangia fedha kwa ajili ya shule za msingi na Sekondari wilayani Rombo ili ziweze kuwa na vyoo salama na pia kuchangia fedha zitakazowezesha kupandisha hadhi ya hospitali ya Huruma wilayani Rombo ili iweze kuwa hospitali ya Rufaa, niwapongeze sana kwa jambo hili lenye manufaa." Amesema Dkt. Biteko


Ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na wananchi katika kujiletea maendeleo ikiwemo kuunga mkono uanzishaji wa maeneo ya huduma za kijamii kama vile Shule, Vituo vya afya n.k


Ameongeza kuwa, Rombo Marathon licha ya kuchangia katika kuboresha huduma za kijamii, washiriki wa ndani na nje ya nchi pia wamepata fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika nyanja mbalimbali ikiwemo za kiuchumi na kijamii.


Dkt. Biteko, amempongeza Mbunge wa Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kwa kuanzisha marathon hiyo ambayo sasa inafanyika kwa mara ya Pili huku akieleza kuwa ubunifu huo unapaswa kuigwa na kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.


Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amepongeza utamaduni  wa watanzania wanaotoka  mkoani Kilimanjaro wa kurudi katika maeneo yao wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka  huku akieleza kuwa kurudi nyumbani kunasaidia kufahamu changamoto zilizopo na kuzitatua akitoa wito kwa wananchi wa maeneo mbalimbali kuwa na utamaduni huo.


Mbunge wa Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa, marathon hiyo itafanyika kila mwaka tarehe 23 Mwezi Desema huku ikiwa na malengo maalum ambayo ni chanya kwa jamii.


Amemshukuru, Dkt. Doto Biteko kwa kuheshimu marathon hiyo na kukubali kushiriki akieleza kuwa ushiriki huo utakuza marathon hiyo na kuiimarisha  si kiwilaya tu, bali kimkoa na kitaifa.


Viongozi mbalimbali waliohudhuria n marathon hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na .Dkt. Tausi Kida, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.


Washindi wa Kilometa 21 katika mbio za Wanawake ni Neema Mswadi (3), Nathalie Elisante (2) na Sara Ramadhan (1).Washindi wa Kilometa 21 Wanaume ni  Agustino Sule (3), Nestory Steven (2) na Chigale Giniki (1)

Comments