Morogoro
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko
amewataka wadau mbalimbali wanaohusika na mapambano dhidi ya UKIMWI nchini kwa
kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kuhakikisha kuwa
wanatenga fedha za kutosha kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI nchini badala
ya kutegemea wafadhili kwa kiasi kikubwa.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati wa Mkutano Maalum wa Wadau wanaoshughulikia Udhibiti wa UKIMWI
Tanzania uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2023 mjini Morogoro na kuhusisha viongozi
wa Serikali, Wadau wa Maendeleo na Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.
"Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya
UKIMWI na nawataka TACAIDS na wadau kuhakikisha mnashirikiana kwa pamoja dhidi
ya mapambano ya Ukimwi kwa kuongeza ushiriki wa wananchi pia" Amesisitiza
Dkt. Biteko
Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Tanzania, kupitia Serikali ya
Awamu ya Sita, imeendelea kuchukua
jitihada mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI ambayo yamepelekea kupungua kwa maambukizi mapya,
kupungua kwa idadi ya vifo vinavyotokana na UKIMWI, mwamko wa watu wanaotumia dawa (ARV)
umeongezeka, maambuki ya Mama kwenda kwa mtoto yamepungua huku lengo likiwa ni
kutokuwa na vifo vinavyotokana na UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
“Tumeshuhudia pia unyanyapaa dhidi ya Watu wanaoishi na
Virusi vya Ukimwi ukipungua, na haya yote yanatokea huku kukiwa na ushirikiano
wa Wadau, hivyo nawapongeza nyote kwa
juhudi zenu,” Amesema Dkt. Biteko
Ameeleza kuwa, pamoja na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa
na Serikali pamoja na Wadau, bado UKIMWI haujadhibitiwa inavyotakiwa, hali
inayoweza kupelekea maambukizi mapya kuongezeka hivyo
ametaka wadau wote wanaohusika kuendelea na juhudi za utoaji afua mbalimbali
zenye lengo la kumaliza UKIMWI.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya
Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dkt. Jerome Kamwela amesema kuwa, Mkutano
huo unalenga kutoa nafasi ya mashaurinao kati ya Serikali na Wadau wake katika
mapambano dhini ya UKIMWI, na kwamba Mkutano
huo ni muhimu
wakati Tanzania ikielekea kufikia lengo la dunia la kumaliza
UKIMWI ifikapo mwaka 2030 ambapo inatakiwa kusiwe na maambukizi mapya ya
UKIMWI, kusiwe na vifo vinavyotokana na UKIMWI pia, kusiwe na unyanyapaa kwa
watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.
Amesema, Mkutano huo unaangalia usimamizi na uwajibikaji wa
pamoja kati ya Wadau na Serikali, kuangalia uendelevu wa kifedha na rasimali,
kuangalia uendelevu wa program za huduma pia mkutano huo utawawezesha wadau
kujadiliana mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza katika mapambano
dhidi ya UKIMWI na namna ya kuzitatua.
Viongozi waliohudhuria Mkutano huo maalum ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Joyce
Ndalichako na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI, Mhe. Stanslaus Nyongo na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,
Adam Malima.
Comments
Post a Comment