DKT. BITEKO AZINDUA MATOKEO YA UTAFITI WA ATHARI ZA UPATIKANAJI WA NISHATI ENDELEVU TANZANIA BARA

 

*Asilimia 72 ya Kaya zote Tanzania Bara zimefikiwa na umeme*


*Usambazaji umeme vijijini wafikia Asilimia 90*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua matokeo ya utafiti wa athari za upatikanaji wa Nishati Endelevu Tanzania Bara kwa mwaka 2021/2022 ambao umeonesha kuwa asilimia 72 ya kaya zote Tanzania Bara zinaishi katika vijiji/mitaa iliyofikiwa na huduma ya umeme.


Dkt .Biteko amezindua utafiti huo jijini Dodoma tarehe 10 Novemba, 2023 katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Petro Lyatuu, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda ambaye ni Kamisaa wa Sensa.


Dkt. Biteko amesema kuwa, lengo kuu la utafiti huo lilikuwa ni kupima upatikanaji wa nishati endelevu na athari ya upatikanaji wake kwa Tanzania Bara. Aidha, utafiti ulikusanya taarifa za matumizi ya nishati, kwa lengo la kuiwezesha Serikali kutathmini na kufuatilia programu mbalimbali za maendeleo, kutunga sera, na pia kufanya maamuzi sahihi ya mipango ya maendeleo kwa kutumia ushahidi wa takwimu.


“Utafiti huu umefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351 Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Takwimu ya Norway (SSB), pamoja na wadau muhimu wa nishati ambao ni Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ambapo utafiti ulifanyika katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.” Amesema Dkt. Biteko


Ameeleza kuwa, kwa Tanzania Bara kufikia asilimia hiyo 72 ya kaya zote zinazoishi katika vijiji/mitaa iliyofikiwa na huduma ya umeme, Serikali imetimiza lengo namba 7 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG 7) linaloelekeza kwamba "Kufikia mwaka 2030 kuwe na uhakika wa upatikanaji wa huduma za nishati nafuu, za kuaminika, na za kisasa kwa wote.


Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, taarifa ya REA ya mwezi Novemba 2023, inaonesha kuwa, jumla ya vijiji vilivyounganishwa na umeme kwa upande wa Tanzania Bara ni 11,079 sawa na asilimia 90 ya vijiji vyote (12,318), aidha Vijiji vilivyobaki (1,239) sawa na asilimia 10 vinatarajiwa kuunganishwa na umeme ifikapo Juni 2024.


Ameongeza kuwa, Serikali imeanza kupeleka umeme katika vitongoji vyote Tanzania Bara ambapo zoezi hilo limeanza mwaka 2023/24 kwa kupeleka umeme katika vitongoji 15 katika kila jimbo.


Vilevile amesema kuwa, Serikali kupitia REA inatekeleza mradi wa kusambaza mifumo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua katika makazi kwenye visiwa 41 vya Mikoa ya Kagera, Lindi, Mara, Mwanza na Rukwa. Serikali pia kupitia REA inatoa uwezeshaji wa kiufundi na kifedha kwa waendelezaji wa miradi midogo ya nishati jadidifu katika maeneo ya vijijini ili kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme vijijini.


Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali inakamilisha Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia

unaojikita katika kutatua vikwazo vyote vinavyokwamisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na lengo ni kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaimarika nchini.


Aidha, amesema kuwa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuhamasisha matumizi ya LPG kwa kuwapatia wananchi mitungi ya gesi na vifaa vyake ambapo katika mwaka 2023/24 Serikali kupitia REA imepanga kutoa kwa wananchi mitungi 200,000 ya LPG na vifaa vyake pamoja na mifumo ya kupikia ya gesi asilia katika taasisi mbalimbali za umma.


Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Biteko amesema kuwa, bado kuna changamoto ya kupatikana kwa nishati endelevu hivyo amewahakikishia wananchi kuwa, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi na za muda wa kati zitakazowezesha kufikia lengo la nishati safi kwa haraka zaidi.

Comments