Dkt. Biteko amtaka Msajili wa Hazina kutoa maelezo ushiriki hafifu wa mashirika ya umma michezo ya SHIMMUTA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amemtaka Msajili wa Hazina nchini kufikia Jumanne Asbuhi awasilishe
maelezo ya kwa nini mashirika mengi ya Umma hayajashiriki Michezo ya SHIMMUTA
yanayoendelea jijini Dodoma, huku ikitambulika kuwa, mashindano hayo
yalianzishwa na Serikali huku mlezi wake akiwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati akifungua
Mashindano ya SHIMMUTA yanayohusisha Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni
Binafsi ambapo awali, Mwenyekiti wa Kamati ya SHIMMUTA, Roselyne Massama
alimweleza Naibu Waziri Mkuu kuwa wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo
ya muitikio mdogo wa Mashirika ya Umma kushiriki mashindano hayo jambo ambalo
linazorotesha mashindano hayo.
"'Viongozi Serikali kama tumekubaliana kufanya jambo
fulani basi tulifanye, na kama tunaona halifai
basi bora tuliache, kuliko tunakubaliana kufanya kitu halafu hatukifanyi; haiwezekani viongozi wote hapa wanalalamika, Katibu Mkuu
analalamika, Naibu Waziri analalamika na mimi nilalamike?, hapana sijaumbwa
hivyo, sioni sababu yoyote ya kutamkika au ya kuandikika, kwamba kuna mashiriki
ya umma 248 na hapa yapo mashirika 57 tu; haiwezekani." Amesisitiza
Dkt.Biteko
Aidha, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa
na Michezo, kuwaandikia barua Makatibu Wakuu wa Wizara ambao Taasisi zao
hazijashiriki michezo hiyo, watoe maelezo kwanini hawajapeleka wafanyakazi
kwenye mashindano hayo na yeye atashauri viongozi Wakuu wa Nchi, hatua za
kuchukua.Vilevile, ameelekeza mashirika yote ya Umma yanayotakiwa kujiunga na
SHIMMUTA kufanya hivyo.
Dkt.Biteko ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuiongoza na kuisimamia vyema Sekta ya
Michezo na kuipa msukumo mkubwa ambao umefanya Taifa kutambulika zaidi duniani
kote akitolea mfano kuchaguliwa kwa Tanzania
kuwa moja ya nchi wenyeji wa michezo ya AFCON mwaka 2027.
Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko ametaka Wafanyakazi nchini
kufanya kazi kwa weledi na kuwahudumia Watanzania ipasavyo kwani Rais,
Dkt.Samia anapima Watumishi kwa kazi zao, anataka kuwe na matokeo katika kazi
hizo na ndio kipimo pia cha uwezo wa
kuwahudumia Watanzania, hivyo lazima wasimamiane, wasibembelezane na wafanye
kazi kwa taratibu zilizopo.
Pia amewataka Watumishi kuweka alama kwa kutoa huduma bora kwa wananchi, watatue
matatizo ya wananchi na Taasisi zao zisiwe kikwazo cha Maendeleo.
Kuhusu ufadhili wa mashindano ya SHIMMUTA NA SHIMIWI,
Dkt.Biteko ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kusimamia suala hilo
ili michezo hiyo ifanyike kwa ufanisi.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria Hafla ya Ufunguzi huo ni
Mhe. Hamisi Mwinjuma, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson
Msigwa, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Rosemary Senyamule,
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Roselyne Massam Mwenyekiti wa SHIMMUTA.
Michezo hiyo ambayo mwaka huu imefikisha miaka 53 kutoka
kuanzishwa kwake na Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere, imejumuisha Taasisi 57
na wanamichezo walioshiriki ni 3478 huku michezo inayoshindaniwa ikiwa ni 12.
Kauli mbiu ya Maonesho hayo Michezo ni Afya na Uchumi:
Tuwekeze kwenye Miundombinu ya Michezo kwa Afya Bora na Uchumi Himilivu! Kazi
Iendelee.
Comments
Post a Comment