Dar es salaam
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko leo
amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa juu wa Chama cha Kikomunisti cha
China (CPC) ukiongozwa na Mjumbe wa
Kamati na Mkurugenzi Mkuu wa Bureau I, Idara ya Oganaizesheni ya Kamati Kuu ya
Chama cha CPC, Ndugu Mao Dingzhi akiwa ameambatana na Balozi wa China nchini
Tanzania, Mhe. Chen Mingjian
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam tarehe 28
Novemba, 2023 ambapo Ndugu Mao Dingzhi pamoja na kumpongeza Dkt. Biteko kwa
kuteuliwa na kuapishwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,
alizungumzia kuhusu uhusiano mzuri ulipo kati ya Tanzania na China na kushukuru
jinsi Serikali ya Tanzania inavyounga mkono Serikali ya China kwenye majukwaa
mbalimbali ya kimataifa.
Pamoja na kuzungumzia miradi ya Nishati, Dkt. Biteko
aligusia maeneo ambayo Tanzania inahitaji ushirikiano kutoka China, ambayo ni
pamoja na kujengea uwezo wataalam kwenye masuala ya utawala na teknolojia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bureau I na Idara ya
Oganaizesheni ya Kamati Kuu ya Chama CPC, Ndugu Mao Dingzhi amesema Chama cha
CPC na Chama cha Mapinduzi (CCM) vimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu tangu
enzi ya Waasisi wa vyama hivyo ambao ni Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mao
Tse Tung na kuongeza kuwa ushirikiano huo unaendelezwa na vyama hivyo hadi
sasa.
Aidha, amepongeza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezeshaTanzania kuwa nchi ya
amani, uhuru wa kutoa maoni, uzalendo na kuheshimu utu wa wananchi wake na
kuahidi kuendeleza ushirikiano kwenye nyanja za uchumi wa kidijitali, masuala
ya kijamii, utamaduni pamoja na elimu.
Comments
Post a Comment