Bukombe yajipanga kumlinda mtoto dhidi ya ukatili

 

Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka halmashauri ya wilaya Bukombe, Anna Athanas akitoa elimu kwa wanafunzi wakike shule ya sekondari Businda juu ya kujikinga na ukatili wa aina mbalimbali kama vile; ukatili wa kingono, kiuchumi,Kijinsia, kisaikolojia pamoja na kutambua sababu zake, matokeo yake na kuwapa mbinu za nini kofanyike na wapi wanatakiwa kutoa taarifa za matendo hayo.


Halmashauri ya wilayani Bukombe imeanza kuweka mkakati wa kumlinda mtoto kuanzia anapokuwa nyumbani, shuleni na njiani ili kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi yao.


Mkakati huo unaohusisha Umoja wa Wazazi na Walimu (UWAWA) ni sehemu ya mradi wa Shule Bora unaofadhiriwa na   Benki ya Dunia ambapo wilayani Bukombe umeanza kutekelezwa hivi karibuni


Mradi huo unajumuisha pia Waratibu Elimu wa Kata, Walimu Wakuu na Wakuu wa shule, Wanafunzi,  dawati la jinsia la polisi, ofisi ya Ustawi, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto ikilenga pia kupunguza utoro na kuboresha lishe mashuleni.


Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe, Lutengano Mwalwiba alisema kuwa watumishi wa halmashauri hiyo wakiwemo maofisa Maendeleo ya Jamii, Wenyeviti wa kamati za shule, walimu wa malezi shuleni pamoja na walimu wakuu tayari wamepatiwa mafunzo jinsi ya kuweza kubaini vitendo vya ukatili kwa wanafunzi pamoja na kuboresha huduma ya chakula mashuleni. Mafunzo hayo yalifanyika Jijini Mwanza hivi karibuni.


Halmashauri hiyo, tayari imeunda kamati zinazojulikana kama Umoja wa Walimu na Wazazi (UWAWA) katika kata za Igulwa, Bulangwa, Katente na Runzewe Mashariki kwa ufadhili wa Bank ya Dunia (WB) ili kusaidia kumlinda mtoto anapokuwa shuleni, nyumbani na njiani dhidi ya vitendo vya ukatili. Lengo ni kuwa na kamati hizo kwa kila kata.


Akieleza jinsi kamati hizo za UWAWA zinavyofanyakazi Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Bukombe (DCDO),  Melania Kwai alieleza kuwa zitasaidiwa na mabaraza ya shuleni kama vile Baraza la Mawasiliano, Malalamiko, Dawati la usalama, Chumba cha unasii na Sanduku la Maoni lenye kufuli tatu.


Hata hivyo, mabaraza hayo yanafanyakazi kwa karibu zaidi na ofisi za ustawi, maendeleo ya jamii, dawati la jinsia na waratibu elimu-kata katika kuhakikisha kulindwa kwa haki ya mtoto wilayani Bukombe!


Mwalimu wa malezi katika shule ya msingi Kasozi na mjumbe katika UWAWA, Hamis John pamoja na hofu ya changamoto ya msimu wa kilimo kwa wazazi alisema leo Novemba 6, 2023 wanakusudia kukutana kwa mara ya kwanza kuweka mikakati kabla matukio ya ukatili hayajaripotiwa shuleni hapo.



Kwa upande wa mzazi, Edmund Migulano ambaye mtoto wake anasoma darasa la tatu shule ya msingi Msonga iliyo katika kata ya Runzewe Mashariki, pamoja na kushukuru uongozi wa shule hiyo kwa kujumuishwa katika kamati ya kumlinda mtoto, UWAWA alieza jinsi ushirikiano wa Wazazi na Walimu ulivyompa wajibu mpya wa kuhudhuria vikao shuleni,  kusimamia usomaji wa wanafunzi nyumbani, kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto,  kuhamasisha uandikishaji wa watoto shuleni, mahudhurio pamoja na ufaulu wa wanafunzi kwenda sekondari, kuboresha miundombinu ya shule na kuimarisha mazingira salama na rafiki ya ujifunzaji ili kuchochea maendeleo ya wilaya ya Bukombe


Akizungumzia changamoto ya baadhi ya wazazi kushiriki katika vitendo vya ukatili ikiwemo kuwanyima watoto haki ya kupata elimu Afisa Maendeleo ya Jamii Msaidizi,Vumilia Mchwampaka alisema elimu zaidi inahitajika ikiwemo kuendeleza Mkakati wa Taifa wa Kuwalinda Watoto (MTAKUWA) dhidi ya ukatili kuanzia ngazi ya kijiji, kata, kitongoji, wilaya hadi Taifa ili kuweza kufanikisha ulinzi hata anapokuwa maeneo ya mtaani.


“Ni lazima tuhakikishe kazi nzuri inayofanywa na serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu katika halmashauri yetu iendane na maadili mema, ikiwemo watoto kupenda kusoma na kupatiwa fursa ya kufanya hivyo pasipo kufanyiwa ukatili wa aina yeyote amabayo yanaweza kuathiri makuzi yake na hata kisaikolojia. Viongozi wa kiroho pia wahimize maadili mema katika jamii ili watu wawe na hofu ya Mungu” alisema Vumilia.


Mbunge wa jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko akisalimiana na wanafunzi jimboni humo

Comments