Umeme Sio Anasa, ni Hitaji la Lazima - Dkt. Biteko






Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema umeme sio anasa bali ni hitaji la lazima kwa wananchi.


Mhe. Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 27, 2023 wakati wa hafla wa uwashaji umeme Kijiji cha Mubaba na Nyantakara vilivyopo Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.


“Nimewaambia REA pelekeni umeme vijijini, tunataka Watanzania wazoee umeme. Umeme sio anasa tena bali ni hitaji la lazima kwa Watanzania,” amesema Mhe. Dkt. Biteko.


Ameendelea kusema kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza kasi  kwenye umeme, na anajali shida za Watanzania, hivyo anatatua changamoto mbalimbali likiwemo suala la umeme.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema Mkoa wa Kagera una jumla ya vijiji 662 ambapo vijiji 512 sawa na asilimia 77.3% vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya awali ikiwemo REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, REA Awamu ya Pili na REA Awamu ya Kwanza. 


Ameendelea kusema kuwa, kwa sasa REA inatekeleza jumla ya miradi mitano katika maeneo tofauti ya mkoa wa Kagera, ambayo ni mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, mradi wa kupeleka umeme pembezoni mwa miji, mradi wa ujazilizi, mradi wa kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo na mradi wa kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.



Comments