SIMBACHAWENE AKOSHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA TASAF BUKOMBE






Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Boniface Simbachawene (MB) amefurahishwa na utekelezaji wa miradi ya Tasaf inayotekelezwa Wilayani Bukombe huku akiwataka wananchi kuendeleza moyo wa kijitolea nguvu kazi katika utekelezaji wa miradi.


" Nimefurahishwa sana kuona jinsi miradi ilivyotekelezwa kwa ubora ule ule ambao serikali imekusudia, hongereni sana."


Pongezi hizo alizitoa tarehe 15 Septemba 2023 wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Ishololo na ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa, ofisi moja ya walimu na matundu 6 ya vyoo katika shule ya msingi Ihulike.


Aidha aliendelea kusema kuwa Bukombe kuna ushirikiano mzuri kati ya wananchi na serikali ndiyo maana mnatekeleza miradi bila mapungufu yoyote.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Mhe.Said Nkumba alisema.


"ufanisi mkubwa unaouona katika utekelezaji wa miradi wilayani Bukombe ni pamoja na wananchi kushilikishwa nguvu kazi kama vile kuchota maji, kuchimba msingi, kusogeza mawe na mchanga."


Naye  Bi. Moshi Ramadhani mwananchi kutoka katika kata ya Lyambamgongo kijiji cha Ishololo ameishukuru serikali kwa  kuwaletea mradi wa ujenzi wa zahanati  kwani walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya na sasa wataipata huduma hiyo karibu.


Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe Lutengano Mwalwiba alisema, katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Kupunguza Umaskini (TPRP 1V) Halmashauri imetekeleza jumla ya miradi 10 ambayo sekta ya Elimu ni 5 na Afya 5 iliyogharimu jumla ya  kiasi cha shilingi 884,024,142.91 na kiasi cha shilingi 224,315,007.68 kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya barabara.

Comments