MAJALIWA: TANZANIA KUWA WAZALISHAJI WAKUBWA WA NISHATI



WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Septemba 20, 2023  amefungua Kongamano la Tano na Maonesho ya Nishati Tanzania na amesema kwamba Serikali imedhamiria kuwa mzalishaji mkubwa na nishati.


“Tunaendelea na utafutaji wa gesi, tunataka tuwe wazalishaji wakubwa wa nishati, tuwe na umeme wa kutosha utakaopatikana kwa urahisi na nafuu na ziada tutauza nje ya nchi.“


Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo baada ya kufungua kongamano hilo la siku mbili linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.


Amesema kuwa Tanzania haitegemei kuzalisha umeme kwa kutumia maji pekee bali inaendelea kuweka mkazo katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati nyingine kama gesi na jua.


Waziri Mkuu amesema katika kongamano hilo la kimataifa la nishati ambalo limehusisha  viongozi na wadau kutoka katika mataifa mbalimbali Duniani litajadili namna bora ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa nishati.


Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa kuzisisitiza nchi zote wanachama kuhakikisha taasisi za mafunzo zinatoa  programu maalum za mafunzo katika sekta za nishati ili kuongeza idadi ya watu walio na ujuzi na maarifa kwenye sekta hiyo.


Amesema kuwa nishati ni sekta muhimu katika kufikia lengo la uanzishwaji wa viwanda na katika kuimarisha na kuwezesha uzalishaji na shughuli nyingine za kiuchumi. “Lazima tufanye kazi kwa ushirikiano na wadau wote ili kufungua fursa kwa Watanzania wote.”


Amesema ili kuwaendeleza wafanyabiaahara wa ndani na Watanzania kushiriki katika sekta ya nishati, Serikali itaendelea kuhakikisha kanuni na taratibu zinazofaa zinawekwa ili kuwezesha ushirikishwaji katika mnyororo wa thamani wa maendeleo kwenye sekta ya nishati


Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema wameendelea kutekeleza mipango mbalimbali waliojiwekea katika kuhakikisha umeme unapatikana wakati wote nchini.


Dkt. Biteko amesema zaidi ya kampuni 100 za nishati kutoka katika maeneo mbalimbali duniani zinashiriki katika kongamano hilo ambalo lilitanguliwa na mkutano wa viongozi wa nishati.







Comments