KAWAFUNDISHENI WENGINE ILI KULETA MABADILIKO YA KIUCHUMI - DED LUTENGANO





Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe amewataka vijana waliopata mafunzo kuhusu Teknolojia ya  utengenezaji wa vihenge vya chuma (metal Silo) kuhakikisha wanatoa ujuzi kwa vijana wenzao ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi ndani na nje ya wilaya ya Bukombe.


Maagizo hayo ameyatoa leo tarehe 7 Sept, 2023 wakati wa ugawaji wa vifaa vya uchomeleaji na uungaji vyuma vilivyotolewa na VETA kwa kushirikiana na Wizara ya kilimo kupitia Mradi wa TANIPAC.


Aidha Lutengano amewataka wananchi kutumia vihenge hivyo kwa ajili ya kuhifadhi mazao ili yasiathiriwe na Sumu Kuvu ( fungus) ambao wanasabisha kansa kwa binadamu na wanyama wanapokula mazao yenye vimelea vya Sumukuvu. 


Vile vile Mhandisi Kapele Kisembe kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) amesema,  VETA ilitekeleza jukumu hilo kwa ufanisi kwa kutoa mafunzo kwa vijana 420 kati ya 400 kutoka katika mikoa 10 waliotarajiwa kunufaika. Vijana walionufaika na mafunzo hayo ni kutoka kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na athari ya Sumukuvu ikiwemo Wilaya ya Bukombe.


Naye Kaimu wa Divisheni  ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (W) Joseph Machibya amesema Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ni wilaya iliyobahatika kupata mafunzo hayo na  jumla ya vijana 20 wamenufaika na mafunzo kutoka katika tarafa zote 3 ambazo ni Bukombe, Siloka na Ushirombo.


David Simoni ambaye ni mnufaika wa mafunzo hayo kutoka katika kata ya Katente  kwa niaba ya vijana wenzie amemshukuru Mhe. Rais DKT. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupata mafunzo pamoja na kugawiwa vifaa vya uchomeleaji.


"Tumepewa vifaa hivi ili tukafanye kazi kulingana na maelekezo tuliyopewa na serikali. Vifaa hivi tunaahidi kuvitunza na kuvitumia vizuri ili kuweza kupambana na  Sumukuvu."


Ugawaji wa vifaa hivyo ulizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  tarehe 8/8/2023 katika kilele cha Maonesho ya Kilimo Nanenane Jijini Mbeya.


Comments