DKT.BITEKO AANZA ZIARA YA KIKAZI BUKOMBE MKOANI GEITA




APATA MAPOKEZI MAKUBWA YA WANANCHI


AAGIZA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA ZA SERIKALI


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko ameanza ziara ya kikazi katika jimbo hilo lililoko mkoani Geita ikiwa ni ziara ya kwanza kufanyika  kutoka ateuliwe na kuapishwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.


Mara baada ya kuwasili katika Jimbo hilo tarehe 24 Septemba, 2023, Dkt.Biteko alipokelewa na wananchi wa Jimbo hilo pamoja na viongozi mbalimbali katika Wilaya Bukombe na Mkoa wa Geita.


Akizugumza  katika Mkutano wa hadhara, Dkt.Biteko amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kuona kuwa anaweza kumsaidia katika majukumu aliyokabidhiwa na kuahidi kuwa, atatekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kuwatumikia wananchi ili kuitendea haki imani iliyooneshwa kwake.


Amesema kuwa, chini ya uongozi wa Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kila kitu kilichopangwa kufanyika  kinaendelea kufanyika kutokana fedha anazotoa katika  miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo mradi wa umeme wa Julius Nyerere (MW 2115), ujenzi wa Daraja wa Busisi, ununuzi wa ndege, madarasa, vituo vya afya, utalii n.k.


Kutokana na hilo, Dkt. Biteko amewataka watendaji na watumishi nchini kusimamia matumizi sahihi ya fedha za Serikali kwani fedha hizo ndizo zinategemewa na watanzania katika kuwaletea maendeleo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa Mkoa wa Geita wamemshukuru Rais,  Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini Dkt.Doto Biteko katika nafasi hiyo kubwa na adhimu na kwamba wana imani kuwa ataitendea haki nafasi hiyo kutokana na historia yake ya uchapakazi na uadilifu.


Viongozi hao wakiwemo Wabunge na Wakuu wa Wilaya katika Mkoa wa Geita wamemshukuru Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara wilayani Chato, ujenzi wa Chuo cha VETA wilayani Nyang'hwale na upelekaji umeme vijijini katika vijiji vya Mkoa huo.


Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesifu juhudi zilizofanywa na Dkt.Biteko wakati akihudumu kama Waziri wa Madini  na kueleza kuwa amesaidia kuinua mchango sekta ya madini katika uchumi wa nchi na ameahidi kuwa ataendeleza misingi hiyo mizuri ikiwemo ya kufanya utafiti wa madini katika eneo lote la nchi ili wachimbaji wachimbe madini kwa uhakika na hivyo kuongeza mapato ya nchi.


Aidha, ameendelea kusisitiza kuwa, hatalifanyia mzaha suala la utoroshaji wa  madini nchini na kwamba wote watakaotorosha madini watachukuliwa hatua za kisheria kwani wanakosesha nchi mapato.


kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan 

 kwa kutoa fedha za kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo shule, hospitali na umeme katika Mkoa Geita.







Comments