DKT. BITEKO AWASIHI WAFANYABIASHARA WA PETROL NA DIZELI KUWA WAAMINIFU.




Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewasihi Wafanyabiashara wa mafuta ya dizeli na Petroli nchini kuwa waaminifu wakati wakiendelea kutoa huduma kwa Watanzania.


Dkt. Biteko  ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Wafanyakazi wa EWURA jijini Dar es Saalam Septemba 14, 2023 na kukukumbushia kuwa, pamoja na kuwa ni Wafanyabishara lakini pia wanatoa huduma kwa Wananchi.


‘’Naomba Wafanyabiashara wenye leseni za biashara ya mafuta nchini watambue kuwa wana wajibu wa kuhudumia watanzania ili wapate bidhaa hiyo, tunajua kuwa kiwango cha uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi kimepungua lakini Serikali inaendelea kulifanyia kazi,” amesema Dkt. Biteko.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Biteko amesema,  Serikali inafanya kazi kubwa ili kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini inamalizika.


Dkt. Biteko ameitaka EWURA kuhakikisha inapitia mfumo mzima wa upangaji wa bei ya mafuta ili kuwezesha bei zinazopangwa zilingane na uhalisia wa maisha.


“Wazalishaji wa mafuta duniani wamepunguza uzalishaji lakini mahitaji ya mafuta yameongezeka kwa sababu ya shughuli za kiuchumi zinazotekelezwa ikiwemo ununuzi wa magari na ujenzi wa viwanda vya kuzalisha malighafi mbalimbali,” amesema Dkt. Biteko.


Aidha, amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo Serikali imeanza kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya  Gesi Asilia - CNG ili kuhamasisha wananchi kuanza kutumia magari yanayotumia mfumo wa Gesi Asilia ikiwemo magari ya Serikali.


Amefafanua kuwa faida zitakazopatika kama magari yaliyokuwa yakitumia mafuta yakianza kutumia mfumo wa uendeshaji unaotumia Gesi Asilia - CNG, gharama za uendeshaji wa magari hayo zitapungua na mafuta yaliyokuwa yakitumiwa na magari hayo yatatumika kuendesha mitambo iliyopo viwandani.  


Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na watendaji wengine kutoka wizara ya Nishati na EWURA.



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko, akiwasili katika Ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), zilizopo  jijini Dar es Salaam, Septemba Leo Septemba 14, 2023



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), leo Septemba 14,2023 jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko (wa kwanza kulia), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha.Felchesmi Mramba (wa nne kulia),  wakiwa na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA

Comments