DKT. BITEKO ATOA SIKU 14 KUANZA UZALISHA WA ALMASI MWADUI



Mgodi wa Uchimbaji Mkubwa wa Madini ya Almasi wa Mwadui kuanza uzalishaji baada ya kusitisha uzalishaji kufuatia ajali ya kubomoka kwa bwawa la tope laini iliyotokea Novemba 07, 2022.


Hayo ameyabainisha na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko baada ya kutembelea Mgodi wa Williamson Diamonds Limited unao milikiwa kwa ubia kati ya Serikali kwa asilimia 25 na Kampuni ya Petra kwa asilimia 75.


Dkt. Biteko ametembelea mgodi huo kwa lengo la kufanya ukaguzi wa ujenzi wa bwawa la kuhifadhia tope laini linalitokana na usafishaji wa mchanga wenye madini ya almasi unaoendelea katika mgodi huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 97 unaotarajiwa kukamilika baada ya siku 14 kuanzia leo Juni 30, 2023.



Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema Sekta ya Madini inaongoza kwa kuuza mazao yake nje ya nchi na kuongeza kuliingizia taifa fedha za kigeni ambapo bidhaa zitokanazo na madini ya dhahabu ikiongoza na kufuatiwa na bidhaa zitokanazo na madini ya almasi.



Aidha, Dkt. Biteko amempongeza Mkoa wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Modest Mkude kwa kufanikiwa kutatua changamoto iliyojitokeza baada ya kutokea kwa ajali ya kubomoka kwa bwawa la tope laini na kusababisha athari kwa jamii inayokuzunguka mgodi huo.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Modest Mkude amesema wananchi 66 walioathirika na tukio la kubomoka kwa bwawa la kuhifadhia tope laini, mgodi umewafidia waathirika 61 sawa na asilimia 98 na wiki ijayo mgodi utakamilisha zoezi la kulipa fidia waathirika 5 waliobaki.


Naye, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Williamson Diamonds Limited, Mhandisi Ayoub  Mwenda amemshukuru Waziri Biteko kwa kuidhinisha kuanza uzalishaji na ameahidi kuto tokea tena ajali ya kubomoka kwa bwawa la tope laini ambapo amesema kwa sasa bwawa hilo limejengwa kwa umahiri mkubwa.


Pia, amesema wananchi wote walioguswa na tukio hilo wamefidiwa na ameahidi kuanza uzalishaji ndani ya wiki mbili kama alivyoagiza Waziri



Awali, Dkt. Biteko alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mdeme kwa lengo la kupata taarifa za shughuli za madini zinazoendelea mkoani humo.

Comments