Dar es Salaam. Wakati Shule za Mikoa ya Kanda ya Ziwa zikiongoza kufungiwa kwa udanganyifu wa matokeo ya mtihani wa darasa la saba, rekodi hiyo ni kinyume na miaka miwili iliyopita kwani kanda hiyo ndiyo iliyoongoza katika ufaulu kwa wakati huo.
Juzi, Necta ilitangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2022, huku ikitangaza kuzifungia shule 24 kwa udanganyifu sawa na asilimia 0.13 ya vituo vyote vya mtihani.
Kati ya shule hizo zilizofungiwa 17 (asilimia 70) zinatoka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, zimo pia zilizowahi kuchomoza katika orodha ya 10 bora ya matokeo ya miaka miwili iliyopita.
Akitaja orodha ya shule hizo zilizofungiwa juzi, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amasi alitaja Kadama ya Geita, Rweikiza (Bukoba), Kilimanjaro shule ya msingi (Arusha) Sahare (Tanga), Ukerewe (Mwanza), Peaceland (Mwanza), Karume (Kagera) na Al-hikma (Dar es Salaam).
Nyingine ni Kazoba (Kagera), Mugini (Mwanza), Busara (Mwanza), Jamia (kagera), Winners (Mwanza), Musabe (Mwanza), Elisabene (Songwe), High Challenge (Arusha), Tumaini (Mwanza), Olele (Mwanza), Mustlead (Pwani).
Pia zipo shule za Moregas (Mara), Leaders (Mara), Kivulini (Mwanza) na St Severine (Kagera).
“Vituo hivi vimefungiwa kwa mujibu wa kifungu 4(8) cha kanuni za mitihani mwaka 2016 hadi hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa mitihani ya kitaifa,” alisema Amasi.
Kwa miaka miwili mfululizo 2020 na 2021 kanda hiyo ilikuwa na rekodi kwa shule zake kuongoza katika matokeo ya mtihani huo.
Mwaka 2020 shule nane kati ya 10 zilizofanya vizuri zilitoka katika kanda hiyo zikiongozwa na God’s Bridge ya mkoani Mbeya, ya pili ni Bunazi Green Acres ya Kagera, Twibhoki ya Mara ilikuwa ya tatu, ilifuatiwa na Kwema Modern ya Shinyanga.
Nyingine Graiyaki ya mkoani Mara, ilifuatiwa na Kemebos na Rweikiza za Kagera, St Anne Marie (Dar es Salaam), Mumtaaz (Mwanza) na Rocken Hill ya Shinyanga.
Kilichotokea mwaka 2020, kimejirudia mwaka 2021 kwa shule nane zilizoongoza kutokea Kanda ya Ziwa.
Kwa mujibu wa Necta, nafasi ya kwanza ilishikwa na Graiyaki ya mkoani Mara, St Peter Claver ya mkoani Kagera nafasi ya pili, Rocken Hill ya Shinyanga ya tatu na Kemebos ya Kagera ya nne.
Nafasi ya tano ilishikwa na Bishop Caeser ya Kagera, ikifuatiwa na Kwema Modern ya Shinyanga, huku St Magret ya Arusha ikiwa nafasi ya saba, Waja Springs ya Geita ikishika nafasi ya nane, ya tisa ilishikwa na Kadama ya Geita na 10 ilikuwa Chalinze Modern Islamic.
Comments
Post a Comment