DKT. BITEKO: WAFANYABISHARA WASIO WAAMINIFU, SABABU WACHIMBAJI KUUZA MADINI NJE YA SOKO



*GST mbioni kusogeza huduma za maabara Chunya*


Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema, pamoja na Serikali kuweka mifumo mizuri ya biashara ya madini, wapo baadhi ya watu wasio waaminifu ambao wanawashawishi wachimbaji kununua madini nje ya soko.



Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara wadogo wa madini ya dhahabu (Broker) katika soko la madini la Mkoa wa Kimadini Chunya ambapo amewataka wafanyabiashara hao kuachana na tabia hiyo.


"Kuanzia sasa tutakuwa tunachambua mwenendo wa kila Broker wakati wa kufanya mapitio ya leseni zao ukifika tutakwenda na wale waliokuwa waaminifu na ambao siyo waaminifu watafute biashara nyingine ili tubaki na watu waaminifu," amesema Dkt. Biteko.



Pia, amewataka wafanyabishara hao kufanya biashara kwa haki na kufuata taratibu ili Serikali ipate haki yake na wafanyabishara wapate haki zao na isitokee upande mmoja upate na mwingine ukose.


 Aidha, Dkt. Biteko amewataka wafanyabiashara wa madini Chunya kutunza kumbukumbu ili kutoka kwenye biashara ya makadirio na kwenda kwenye biashara ya kufuga vitabu na mwisho wa siku kuwa wafanyabiashara wakubwa.



Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST) iko mbioni kusogeza huduma za kimaabara katika Mkoa wa Kimadini wa Chunya kwa ajili ya kusaidia wachimbaji kupima sampuli za udongo na miamba ambapo amekagua ujenzi wa ofisi ya maabara ya GST unaoendelea wilayani Chunya.


Aidha, Dkt. Biteko amekagua shughuli za uchimbaji madini katika migodi ya Imuma Investment Company Limited, Singa Duwila na mgodi wa Frank Mbwilo iliyopo katika kijiji cha Sangambi wilayani Chunya ambapo amewapongeza kwa uchimbaji wa kisasa wanaoufanya.



Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amefanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Majengo wilayani Chunya kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wadogo wa madini zinazowakabili katika shughuli zao.


"Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuagiza kuja kutatua changamoto na si kuondoka na changamoto, ameniambia tuhakikishe kero mlizonazo wachimbaji wadogo zinaisha kama siyo kupungua kabisa," amesema Dkt. Biteko.


Naye, Mbunge wa Jimbo la Lupa lililopo wilaya ya Chunya mkoani Mbeya Masache Kasaka amempongeza Dkt. Biteko kwa kufanya ziara wilayani humo na kuamba Serikali isaidie kusambaza nishati ya umeme katika maeneo ya uchimbaji madini katika wilaya hiyo.

Comments