Malima Atoa Siku Saba aliyeua Albino Kwimba akamatwe*



Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amefika kwenye kijiji cha Ngulla kuwapa pole Bi. Minza Marco (Mjane wa Marehemu), wananchi na wanafamilia kufuatia Kifo cha kikatili cha Ndugu Joseph Mathias (50) kilichotokea usiku wa tarehe 02 Novemba, 2022 baada ya watu wasiojulikana kumkata Mkono wa Kulia na kusababisha kifo chake.


Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ngulla leo (Novemba 03, 2022) alipofika kijijini hapo kuwapa pole, Malima amewahakikishia famila hiyo kuwa Serikali itahakikisha watuhumiwa waliofanya tukio hilo wanasakwa na kukamatwa popote walipo na watachukuliwa hatua kali za kisheria.



"Hili jambo ni baya sana na limetutia doa hivyo naliagiza jeshi la Polisi na vyonbo vingine ndani ya wiki moja wanieleze ni kitu gani kilitokea hapa maana wanaoamini kwamba unaweza kutengemeza maisha kwa viungo vya watu wengine naamini walishakwisha ila leo imenidhihirishia kwamba bado mambo haya yapo kwenye jamii." Malima.


Aidha, Malima ametoa Tshs. Milioni Moja kwa familia hiyo kama Ubani na amewataka kuwa na Subira na Imani katika kipindi hicho kigumu cha huzuni na kwamba mamlaka zinazohusika zinaendelea ma uchunguzi wa mwili na ifikapo ijumaa ya tarehe 04, 11, 2022 watakabidhiwa mwili ili kuweza kumzika. 



"Hatuwezi kumrudisha mume wake, ila mkono wa sheria utafuata Mkondo wake na hatutawaacha wahuni hao na kuruhusu wakitembea kwenye ardhi ya Mwanza lazima watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria," asema Malima.


Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Ngulla na vijiji vya jirani kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na vyombo vingine vinavyohusika na uchunguzi kusaidia kutoa ushahidi wa wanachokifahamu kufuatia jambo hilo ili waliotekeleza wanachukuliwe hatua kali za kisheria na kulikomesha.


"Ndugu zetu hawa wenye ulemavu wa ngozi wana haki ya kuishi ndani ya Mkoa wa Mwanza bila kubughudhiwa na mtu yeyote na hawa Mabwana (Kamati ya Usalama) wakishindwa kuwapata waliofanya tukio hili nitamwomba Mhe. Rais awaondoe wote maana watakua hawatoshi." Amesisitiza Malima. 


Kaimu Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa ACP Mairi Makori amesema Marehemu amefariki Majira ya Saa 5 Usiku akiwa amelala na Mke wake nyumbani kwake kwenye kijiji cha Ngulla ambapo aliitwa na Mtu aliyefika nyumbami hapo na na kugonga mlango huku akimwita jina afungue Mlango na alipotoka nje alishambuliwa na kukatwa Mkono wa kulia.


Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ulemavu Mkoa, Alfred Kapole ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuua Albino kwani jambo hilo ni baya sana na linatia hofu sana kwa wanachi wenye ulemavu huo na ametoa rai kwa mamlaka husika kuchukua hatua kali za kisheria kwa aliyetekeleza suala hilo.


"Sisi tumeumbwa kwa mfano wa Mungu na wala haijulikani kwamba Mungu alimuumba mtu wa aina gani kwa mara ya kwanza hivyo naomba tumrudie Mungu lakini pia nasi tubaki kuwa salama maana sasa tutaanza kuomba fedha za kuendesha maisha kwa kuhofia kwenda shambani kulima." Kapole.

Comments