DC SHIMO AIPONGEZA RUWASA WILAYA YA GEITA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI.

 


Mkuu wa wilaya ya Geita Wilson Shimo ameipongeza Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Geita katika usimamizi imara wa miradi mbalimbali ya maji katika wilaya hiyo. 


Amesema hayo katika Mkutano Mkuu wa nusu mwaka kwa vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO’s) wilaya ya Geita kilichofanyika katika ukumbi wa Alphendo wilayani humo.


Shimo amesema RUWASA inasimamia vyema miradi mbalimbali ya maji katika wilaya hiyo hali inayochangia kuongezeka kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji vijijini katika Wilaya hiyo.



Amevitaka vyombo vya watoa huduma za maji ngazi ya Jamii (CBWSO’s) Kuhakikisha wanasimamia na kuvihifadhi vizuri vyanzo vya maji ili viweze kuwa endelevu na salama kwa watumiaji.


Meneja wa RUWASA wilaya ya Geita Mhandisi Sande Batakanwa amesema Mkutano huo na Vyombo vya watoa huduma ya maji Ngazi ya jamii umelenga kuwajengea uwezo wasimamizi wa (CBWSO’S) Katika jamii ili waweze kusimamia vyema vyanzo vya maji.


Mhandisi Sande amesema RUWASA inashirikiana Vyema na vyombo vya watoa huduma za maji ngazi ya Jamii (CBWSO’s) katika kutunza na kulinda vyanzo vya maji katika wilaya hiyo ili wananchi waweze kupata Huduma ya kutosha ya maji safi na salama.



Mhandisi Sande amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa nyingi za utekelezaji wa miradi ya maji katika wilaya hiyo zilizowezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maji kwa lengo la kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.


Amesema kutokana na kupata pesa za kutosha katika utekelezaji wa miradi ya maji umewezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maji ikiwemo mradi wa maji kata ya Izumacheli wilayani humo ampapo tangu uhuru hakukuwa na huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.



Amesema mpaka sasa upatikanaji wa maji Geita vijijini umefikia asilimia 57 huku RUWASA wilaya ya Geita inaendelea kutekeleza miradi zaidi ya sita inayoendelea na pindi itakapo kamilika itawezesha kuongezeka kwa hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 57 hadi kufikia asilimia 65.

Comments