WAZIRI JAFO AITAKA STAMICO KUONGEZA UZALISHAJI WA MKAA MBADALA


 

Dkt. Jafo Awataka wachimbaji wadogo kutunza mazingira*


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Suleiman Jafo amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuongeza uzalishaji na usambazaji wa mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe ili kuokoa mazingira.


Dkt. Jafo ameyasema hayo alipotembelea  Maonesho ya 5 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini 2022 yanayoendelea mkoani Geita.



Katika ziara hiyo, Dkt. Jafo alianza kwa zoezi la  kupanda miti  ambapo ameipongeza STAMICO kwa kuja na ajenda ya matumizi ya mkaa mbadala ambao ni  rafiki kwa mazingira na umeonesha kuwa mwarobaini wa matumizi ya mkaa utokanao na miti.


Dkt. Jafo ameitaka STAMICO  kuongeza uzalishaji wa Mkaa Mbadala ili uweze kupatikana kwa urahisi kwa Watanzania wote na kushauri STAMICO kuwawezesha vikundi mbalimbali  kwa kuwapa mashine za kuzalisha Mkaa Mbadala ili na wao waweze kuzalisha Mkaa huo na kuusambaza maeneo mbalimbali kwa urahisi zaidi na kujipatia ajira.


Dkt Jafo pia ameishauri STAMICO kuendelea na zoezi la kutafuta Mawakala ili waweze kuanza kuuza katika  maeneo mengi nchini  mara baada ya uzalishaji mkubwa wa mkaa huu utakaponaza.



Aidha, ameitaka STAMICO kuwa mkombozi wa kuokoa rasilimali miti kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ili kufanya kwa pamoja kampeni mbalimbali za kuzuia ukataji miti hovyo na badala yake kuhamasisha  matumizi ya mkaa mbadala.


Ameshauri  Vyombo vya Ulinzi, Mashule, Vyuo na Taasisi zenye kutumia Mkaa wa kuni kuanza kutumia Mkaa Mbadala kama suluhisho la kupikia ili kuondokana na utumiaji wa kuni na akashauri waanze kuwasiliana na STAMICO ili kujua jinsi Mkaa Mbadala unavyofanya kazi.


Aidha ameiagiza Geita Gold Mine Limited (GGM) na STAMICO  kuwawezesha wajasiliamali kwa kununua miche 700 ya miti kutoka kwa mjasirialia mali  Ruthberta Supply anayezalisha na kuuza Miche kwa ajili ya kupanda kwenye Mashule na Hospitali zilizoko Geita ili na yeye aweze kujipatia kipato.



Pia, Dkt. Jafo ametoa wito kwa wachimbaji wadogo wa madini na wadau wote wa madini nchini kutunza mazingira kwa lengo la kuepuka athari za mazingira.


Pamoja na mambo mengine, Dkt. Jafo ameipongeza STAMICO  kwa kutengeneza  mazingira  wezeshi ya kutunza mazingira kwa wachimbaji wadogo kwa kutengeneza vituo vya mfano vya wachimbaji  vinavyohamasisha matumizi ya kemikali zisizo na madhara makubwa kwa watumiaji.


Jafo amesema matumizi ya miti kwa lengo la kukwepa gharama za matumizi ya chuma kuwa ni miongoni mwa sababu za uharibifu wa misitu unaofanywa na wachimbaji wadogo.


Miongoni mwa madhara hayo ni kupotea kwa uoto wa asili, ukame, kukauka kwa vyanzo vya maji, kukosa mapato yatokanayo na uhifadhi na mwishowe umaskini.


Katika hatua nyingine, Dkt. Jafo ameipongeza STAMICO kwa kuendelea kuwalea wachimbaji wadogo wa madini nchini.









Amewataka wadau wote wa madini kufika katika maonesho hayo ili kujifunza namna bora ya matumizi ya teknolojia ikiwemo matumizi ya chuma badala ya miti.


Maonesho hayo ya Madini yanatarajiwa kufugwa rasmi tarehe 8 October 2022.

Comments