WATUMISHI MADINI WATAKIWA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI KUVUTIA UWEKEZAJI



Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake wametakiwa kuweka mazingira wezeshi kwenye maeneo yao ya kazi yatakayovutia uwekezaji katika sekta ya Madini ili hatimaye Serikali iweze kunufaika na kupata mapato stahiki yanayotokana na rasilimali Madini.



Hayo yameleezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Adolf Nduguru kwa niaba ya Waziri wa Madini wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika mkoani Morogoro na kutanguliwa na mkutano wa mafunzo kwa wajumbe wa baraza hilo.


Ameongeza kuwa, kwa kufanya hivyo kutaiwezesha sekta ya Madini kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa na kufikia mchango wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2022 kama ilivyo ainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa .



Amesema kuwa, ili kufikia asilimia hiyo ni lazima wawepo wawekezaji na kwamba lengo hilo litafikiwa kikamilifu kwa watumishi kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi katika maeneo yao ya kazi ikiwemo kuhakikisha huduma wezeshi za kiuwekezaji zinatolewa, leseni zinatolewa, pamoja na mazingira mengine ambayo yatawezesha kutoa matokeo mazuri na hivyo kuchochea uwekezaji zaidi.



‘’Sheria ya Madini iko wazi, wawekezaji siyo wahisani, kama tunavyojua Serikali inapata mapato yake kupitia kodi na mirabaha. Aidha, kwenye uwekezaji mkubwa na wa kati kama serikali tuna hisa za asilimia 16 ambazo hazipungui thamani,’’ amesisitiza Katibu Nduguru.


Pia, amesema kuwa, kama watumishi wa umma, wanao wajibu wa kutekeleza majukumu yao na kusimamia sekta ya Madini kwa uzalendo, weledi, uaminifu na ufanisi ili kutimiza matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan ya kuona sekta ya Madini inalinufaisha taifa na watanzania kutokana na rasilimali ambazo nchi imejaaliwa kuwa nazo.



Ameongeza kuwa, kushiriki katika mkutano huo, kunatoa fursa ya kujitathmini na kupima mwenendo wa utekelezaji wa majukumu baada ya kutekeleza bajeti katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.


Akisoma risala fupi Katibu wa Chama Cha Watumishi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini Cecilia Mrope ameipongeza wizara kutokana na mafanikio kadhaa yaliyopatikana na kuiomba wizara kuona umuhimu wa kuwakutanisha wataalam wa wizara na taasisi ili kujadili masuala makubwa yatakayoiwezesha wizara kuongeza migodi, mapato, kubuni miradi chochevu na kukwamua iwaipo miradi iliyokwama kuanza.  


Awali, Mjumbe wa TUGHE kutoka Makao Makuu Taifa Dennis Tosiri ameipongeza wizara ya madini kutokana na namna inavyoshughulikia changamoto za watumishi na kuongeza kuwa, kutekelezwa kwa changamoto hizo katika maeneo yao kunasaidia kuongeza tija na ufanisi wa kazi.



Pia, ametaka Tughe tawi la wizara kuhakikisha linaongeza idadi ya wanachama na kueleza kwamba suala hilo litakiwezesha chama kuwa imara na kusaidia masuala mengine kuendelea.


Katika Mkutano huo, wajumbe wa baraza wamepata fursa ya kupokea taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ya wizara ikiwemo taarifa ya matumizi na mwenendo wa matumizi ya Bajeti kwa robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2022/23 na taarifa nyingine.




Aidha, katika mkutano huo, wizara imetumia kutoa vyeti vya kutambua mchango wa watumishi kadhaa wa wizara waliostaafu na ambao wanatarajia kustaafu kwa mujibu wa Sheria katika kipindi cha mwaka 2022/23.


Vilevile, wizara imetumia nafasi hiyo kumpongeza mtumishi wa wizara Nyamwiza Ndibalema ambaye alipata medali tatu moja ikiwa ya dhahabu na mbili za shaba kutokana na kushinda mbio za mita 3,000, 1500 na mita 800 katika mashindano ya Shirikisho la Michezo la Wizara, Taasisi na Idara za Serikali (SHIMIWI) yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Tanga.

Comments