TRA GEITA YAWAPA ELIMU WAFANYABIASHARA NYANG'HWALE




Wafanyabiashara wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita wametakiwa kusajili na kurasimisha biashara zao kwa lengo la  kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) hali itakayowasaidia kukidhi vigezo vya kupata tenda mbalimbali katika makampuni ndani na nje ya Mkoa wa Geita.


Rai hiyo imetolewa na ofisa elimu na huduma kwa mlipa kodi  kutoka Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Geita Justine Katiti wakati akizungumza na , wafanyabishara hao Busolwa na Kharumwa wilayani  Nyang'hwale.



Katiti amesema wafanyabiashara wanapaswa kuwa na kasumba ya kuweka kumbukumbu za biashara zao ili kuwawezesha kupata  fursa mbalimbali ikiwemo kupata fursa ya  kukopesheka kwenye taasisi za kifedha pindi wanapokuwa na taarofa zao sahihi za biashara zao.


Amesema katika kutunza kumbukumbu sahihi za biashara wanazozifanya wafanyabiashara hao wanapaswa kutumia mashine za Kielektroniki za Risiti (EFD) kwa lengo kuepuka kufanya makadirio yasiyo sahihi na yenye udanganyifu katika biashara zao.



Nao baadhi ya wafanyabiashara wilayani Nyang'hwale wameipongeza mamlaka ya mapato nchini (TRA) Mkoa wa Geita kwa kuwapatia elimu itakayowasidia katika kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika biashara zao kwa lengo la kuongea ukusanyaji wa mapato hali itakayosaidia serikali kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato.

Comments