TRA MKOA WA GEITA YAKEMEA UPOTOSHAJI WA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI


MAMLAKA ya Mapato Nchini (TRA) Ofisi za Mkoa wa Geita, imewataka wafanyabiashara kuondoa dhana potofu juu ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) badala yake wanapokidhi vigezo wasajiliwe ili kupata fursa za kiuchumi.


Kauli hiyo inakuja baada taarifa kuonyesha baadhi ya wafanyabiashara waliotimiza vigezo wamekuwa hawana uelewa juu ya VAT na kukwepa kusajiliwa pasipo kujua kodi hiyo inalipwa na mteja na inatoa fursa ya kupata tenda kwa makampuni.


Akizungumza katika maonesho ya Fahari ya Geita yanayoendelea katika viwanja vya ccm kalangalalala mkoani Geita  Ofisa Huduma Elimu kwa Mlipa Kodi TRA Ofisi za Geita, Justine Katiti alisema VAT haiongezi gharama ya kodi bali inalipwa kwa thamani ya faida ya utoaji huduma kwa mteja.


“Niwaondoe hofu wafanyabaishara kwamba ukisajiliwa kwenye VAT kwamba kunaongeza gharama, (ya kodi) hamna gharama yeyote, sanasana inamupa nafasi mfanyabiashara atakapokwenda kunua bidhaa mfano pikipiki atakapokwenda kununua pikipiki atalipa VAT kule.


“Atakapokuja kuuza ile pikipiki atajirejeshea kwanza ile VAT aliyolipa kule alipokwenda kununua ule mzigo kwa hiyo ni faida kwamba, unapokuwa umesajiliwa kwenye VAT unapouza ile bidhaa unajirejeshea kwanza ile gharama ya VAT” alisema Katiti


Alisema wafanyabiashara hawapaswi kuamini kwamba wanapolipa tozo za serikali na VAT wanalipa kodi zaidi ya mara moja kwa kuwa VAT inalipwa na mteja anaponunua bidhaa.


Katiti aliwataka wafanyabiashara kuendelea kufanya biashara kwa miongozo ili kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha huduma za kijamii kwakuwa kodi inayotozwa inarejea moja kwa moja kwenye huduma za kijamii.

Comments