MKOA WA GEITA WAENDELEA KUWA KINARA KWENYE SEKTA YA MADINI



Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda amesema kuwa mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa madini hususan madini ya dhahabu, ambapo unachangia zaidi ya asilimia 35 ya mapato yote yatokanayo na shughuli za madini nchini yanayokusanywa na Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini.


Amesema hayo leo (10.02.2022) baada ya timu ya wataalam kutoka Tume ya Madini na Imaan Media kutoka Morogoro kutembelea Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na kujionea shughuli mbalimbali za madini zinazofanyika ikiwemo uchimbaji, uchenjuaji, na biashara ya madini.


“Kama ishara ya wingi wa shughuli hizo za uchimbaji, tunazo leseni za madini 1600 kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Geita, leseni za Uchimbaji wa kati 14 na leseni za Uchimbaji mkubwa 2, ambapo moja ya leseni kubwa inamilikiwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM)" amesema Mapunda.



Katika hatua nyingine Mapunda ameeleza kuwa kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini hasa kwenye Mkoa wa Geita kumekuwa na mafanikio makubwa kwenye Uchimbaji mdogo wa madini, ambapo wachimbaji walikuwa na changamoto ya mahali pa kuuzia madini 


Amesema kuwa, masoko hayo yamechangia sana kwenye ukusanyaji wa maduhuli kupitia shughuli zinazofanywa na wachimbaji wadogo wa madini katika mkoa wa Geita.


“Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lengo la makusanyo kwa mkoa mzima ni bilioni 220 na hadi kufikia mwezi Februari 08,2022 imekusanywa bilioni 114 na Tume ya Madini ambapo matumaini ni kufikia lengo ifikapo mwezi Juni 2022, kwa jitihada mbalimbali zinazofanywa kwenye usimamizi wa shughuli za madini katika Mkoa wa Geita," amesema Mapunda.


Naye mfanyakazi wa kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) Mussa Shunashu amesema kuwa mgodi umefanya shughuli mbalimbali kwenye jamii ikiwemo mradi wa kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi katika shughuli za ushonaji, utengenezaji wa sabuni na uchomeaji.


Ameongeza kuwa mgodi umetoa kipaumbele katika kilimo kwa kujenga ghala ya kuhifadhia zao na kiwanda cha kuchakata kuongeza thamani ya zao la alzeti.


“Kampuni ya GGM imegharamia ujenzi wa shule ya Sekondari ya wanawake ya Nyamkumbu mchepuo wa Sayansi kwa asilimia 100 pamoja na nyumba za waalimu lengo likiwa ni kuwawezesha wanawake kwenye suala la elimu, alisema Mussa”.


Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Uchorongaji na Baruti kutoka GGM, Alex Katalyeba ameeleza namna shughuli za uchimbaji wa wazi zinavyofanyika kwa kuzingatia usalama na namna vifusi vinavyopakiwa na kupelekwa eneo husika.


Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, tawi la Geita CPA. Ally Abdu ameushukuru mgodi wa GGM kwa kufadhili kujenga chuo hicho kupitia fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii (CSR) katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya Halmashauri ya Mji Geita, ambapo mgodi ulichangia zaidi ya milion 170 kwenye ujenzi wa Chuo hicho.




Comments