Tume ya Madini kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki ukusanyaji maduhuli madini ujenzi na ya viwandani

 


Matumizi ya mfumo wa Usimamizi wa madini ujenzi kwa njia ya kielektroniki utaanza kutumika rasmi tarehe 25.11.2021 kwa ajili ya kutunza taarifa sahihi za mauzo na Ukaguzi wa Uzalishaji wa Madini Ujenzi.


Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba tarehe 4.11.2021  wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya mfumo wa Madini ujenzi na viwandani yaliyofanyika Katika Chuo cha Madini Jijini Dodoma.


Mafunzo haya yameandaliwa na Idara ya Leseni na TEHAMA kwa Wasimamizi wa Madini Ujenzi kutoka Ofisi za Maafisa Madini Wakazi kuhusu matumizi sahihi ya mashine za  Kielektroniki (POS) kwa ajili ya kusaidia Serikali katika ukusanyaji wa mapato.


Amesema mafunzo haya ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Madini, Doto Biteko Katika ziara yake ya kikazi mkoani Kagera mnamo tarehe 7.10.2021 alielekeza kuanza kutumia rasmi mfumo wa Kielektroniki (POS) katika ukusanyaji wa maduhuli kwenye Madini Ujenzi na Viwandani.


Pamoja na hilo baadhi ya mikoa ilikuwa imeshaanza kutumia mfumo huo (POS) katika ukusanyaji wa maduhuli ikiwa ni pamoja na mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Mara, alieleza Samamba.


Mhandisi Samamba aliendelea kuwasihi Wasimamizi wa Madini Ujenzi kutoka Ofisi za Maafisa Madini Wakazi kuendelea kusimamia ipasavyo maeneo yao na kuelimisha wengine juu ya matumizi sahihi ya POS bila kutumia nguvu.


“Tunawategemea mfanye kazi kwa bidiii, huu ndo muda wa kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya kufanikisha malengo ya Tume ya Madini ili kufikia tarehe 25.11.2021 tuwe tumefikia asilimia 80 ya ofisi zinazotumia mfumo wa POS, alisema Mhandisi Samamba.”


Tuna malengo ya kukusanya shilingi Bilioni 650 kwa mwaka fedha 2021 - 2022 ni ongezeko kubwa ukilinganisha na makusanyo ya mwaka jana, Serikali ina Imani na Tume ya Madini na Wizara ya Madini katika kuhakikisha tunakusanya fedha hizi kwa ajili ya kusaidia Sekta ya Elimu, Afya na Miundombinu.


Aidha, aliwaeleza wasimamizi wa Madini Ujenzi na Viwandani kuwa watapewa mafunzo ya matumizi sahihi na utunzaji bora wa mashine za kupimia madini ya metali (XRF).


Akihitimisha hotuba yake fupi, Mhandisi Samamba alisema Mh. Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuendelea kujikinga na maradhi yanayotukabili kama vijana ili tuendelee kuwa na nguvu kazi Katika kujenga Taifa letu.





Comments