Mtendaji Mkuu wa TANGOLD CORPORATION Stephen Mullowney akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya Mgodi wa Buckreef kwa Waziri Biteko Jijini Dodoma
WAZIRI wa Madini, Doto Biteko amesema, Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Buckreef itazalisha ajira nyingi kwa wananchi wa Mkoa wa Geita na Watanzania kwa ujumla mara baada ya uzalishaji mgodini hapo kuanza.
Waziri Biteko amesema hayo leo Novemba 8, 2021 kwenye kikao chake na Uongozi wa Kampuni ya Buckreef (Buckreef Gold Company) kilicholenga kupokea taarifa ya maendeleo ya shughuli za uchimbaji wa dhahabu kilichofanyika katika ukumbi wa Prof. Mruma jijini Dodoma.
Amesema, mgodi wa Buckreef tayari umetoa ajira zaidi ya 200 ambapo hadi sasa watanzania wengi wameajiriwa kwenye maeneo yanayozunguka eneo la mradi huo. Biteko amesema Mgodi wa Buckreef unaendelea kutoa ajira nyingi ingawa bado uzalishaji rasmi haujaanza.
Akizungumzia mgodi wa Buckreef, Waziri Biteko amesema shughuli za uzalishaji katika mgodi huo zilisimama kwa muda mrefu na wabia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limefanya kazi kubwa ya kuhakikisha miradi yote ambayo ilisimama imeanza kufanya kazi ukiwemo mgodi wa Buckreef.
“Tunaamini kwamba mradi huu utakapoanza utawasaidia watu wa Geita kupata ajira lakini utatuwaongezea mapato wananchi wa eneo hilo.
"Ninatoa wito kwa mgodi kuchangamkia fursa waharakishe mchakato wa leseni lakini barabara ya kutoka Katoro na kwenda eneo la mgodi ni mbaya sana waitengeneze ili watu wa kule wajue kwamba kuna mgodi,” amesisitiza Waziri Biteko.
Aidha, Waziri Biteko ameeleza kuwa tayari Kampuni ya Buckreef imeanza kulipa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha mradi huo.
Amesema, kiasi cha Shilingi Bilioni 6 kimelipwa kwa ajili ya kuwataka wananchi kupisha ili mradi huo uendelee.
Kuhusu utoaji wa huduma za jamii (CSR), Waziri Biteko amesema, Halmashauri ya Mkoa wa Geita sasa imeanza kupokea fedha za CSR kutoka katika mgodi wa Buckreef pamoja na kwamba uzalishaji haujaanza rasmi.
“Wameshatoa fedha za CSR zaidi ya Milioni 350 kwa ajili ya kutoa huduma katika yale maeneo,” amesema Biteko.
Pia, Waziri Biteko amesema Wizara itaendelea kuwapa ushirikiano kwa kila jambo linalohitajika huku akisisitiza kwamba wataendelea kusimamia Sheria ya Madini ili ndoto ya ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba wawekezaji wanakuja na kufanya kazi katika mazingira mazuri yaonekana kwa vitendo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANGOLD, Stephen Mullowney ameishukuru Wizara kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kila hatua ili kufanikisha shughuli za uchimbaji wa madini ya Dhahabu.
Mullowney ameeleza taarifa ya maendeleo ya Buckreef na mpango kazi wao kuanzia utoaji wa fidia, uzalishaji, uchorongaji, ushirikishwaji wa wananchi katika huduma za kijamii pamoja na ushiriki katika matamasha mbalimbali hapa nchini.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Migodi na Huduma za Kihandisi- STAMICO Mhandisi Moses Kongola ameeleza kuwa, shughuli nyingi za manunuzi ya vifaa mbalimbali yatafanyika hapa nchini ili kuhakikisha manufaa ya uwekezaji yanabaki kuwa ya watanzania.
Kampuni ya Dhahabu ya Buckreef ikishirikiana na mbia mwenza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) inajishughulisha na uchimbaji wa madini ya Dhahabu katika Mkoa wa Geita. Vile vile kampuni ya Buckreef inamiliki hisa kwa asilimia 55 na STAMICO inamiliki hisa asilimia 45.
Kikao cha kupokea taarifa ya maendeleo ya shughuli za uchimbaji katika mgodi wa Buckreef, kimehudhuliwa na Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba, Kamishna wa Madini na Dkt. Abdulrahman Mwanga na Afisa Mkuu wa Uendeshaji TANGOLD Andrew Cheatle.
Comments
Post a Comment