Serikali haitorudi nyuma biashara ya tanzanite kufanyika Mirerani





Serikali imesema haitarudi nyuma kufuatia uamuzi wake iliyoutoa awali wa  kuhamishia shughuli za uthaminishaji na biashara ya madini ya tanzanite Mirerani, eneo ambalo ndiko madini adhimu ulimwenguni yanapatikana.


Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko wakati akizungumza na wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa madini pamoja na wachimbaji wa madini waliopo katika mji wa Mirerani, wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara tarehe 24 Septemba, 2021.


Waziri Biteko alisema, inauma sana kuona wananchi wanaoishi katika eneo lililojaliwa kuwa na rasilimali wanaishi katika umaskini ilihali watu kutoka maeneo mengine wananufaika kwa kuchukua utajiri huo na kwenda kunufaisha maeneo yao.


Alisema ili kukuza Sekta ya Madini kunahitaji wadau watakaowekeza katika sekta hiyo huku akitoa mfano wa namna mji wa Geita ulivyokuwa duni kabla ya kujengwa kwa soko la madini tofauti na hali ilivyo sasa ambapo biashara ya madini inafanyika mkoani humo.


Dkt. Biteko aliwataka wafanyabiashara wa madini ya tanzanite kuutendea haki mji wa Mirerani kwa kukubali na kuanza kutekeleza agizo la serikali la kuwataka kuhamishia shughuli zao katika mji huo.


Akizungumzia uamuzi wa ujenzi wa ukuta wa Mirerani Dkt. Biteko alisema wapo baadhi ya wadau waliokuwa wakipinga na kuona ujenzi huo kama kupoteza rasilimali lakini sasa wanaona manufaa ya ukuta ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na biashara ya  madini ya tanzanite.


"Hakuna jambo linalouma kama watu wa eneo fulani wamezaliwa hapo halafu wageni wanakuja na kubeba rasilimali na kukuza miji mingine, tuwatendee haki watu wa Mirerani kwa kidogo wanachofanya wanufaike  na mji ukue", aliongeza Dkt. Biteko.


Alisema, tufanyie utalii wa madini ya tanzanite Mirerani na kuacha kuigeuza Mirerani shamba la bibi, "ningependa Arusha iendelee lakini tufanye biashara kwa haki", alikazia Dkt. Biteko.


Akizungumzia suala la kuongeza muda kwa wafanyabiashara kuhamishia shughuli zao Mirerani Dkt. Biteko alisema changamoto zinazokwamisha kuhamia huko zichukuliwe kama fursa na kueleza changamoto hizo zitatatuliwa taratibu na kwamba  hazitaisha leo na kuwataka kufanyiakazi maelekezo yaliyotolewa na serikali.


"Mafanikio yanakuja polepole, Mirerani mtakuja na pataboreka polepole, polepole mtachukiana na  uzee utawakuta polepole, polepole nitawambia ukweli polepole ili nisije nikalaumiwa kwa kutokuwaeleza ukweli" Alikazia Dkt. Biteko.


Aliendelea kusema, Arusha itaendelea kuwa hub ya kibiashara, dhambi iko wapi tukikapitolaizi madini mengine Arusha na Madini mengine Mirerani.


Aidha, Waziri Dkt. Biteko aliwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kupendana katika kazi na kuacha kutuhumiana na kusema wakiachana na tabia ya kutuhumiana watajenga na kukuza sekta. 


"Mmejaribu miaka mingi sana kuchimba kwa kusemana kila anayefanikiwa Mirerani ni mwizi amini kuwa na wewe utakapofika hatua fulani na wewe utakuwa mwizi, wachimbaji pendaneni mfanikiwe, hawawezi mmewapima saa ngapi?" Alihoji Dkt. Biteko.


Dkt. Biteko amebainisha kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza kuwavuta  watu ili walete mitaji na kuwekeza nchini hivyo tusiwapinge wanaotafuta wawekezaji wenza kuwekeza kwenye biashara ya tanzanite.


Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro,  Ole Sendeka aliusifu uongozi mzuri wa Waziri Dkt. Biteko na kusema kila mara anapomlilia kwa changamoto za wananchi wake zilitafutiwa ufumbuzi.


"Nilikuomba ukaguzi wa staha ulipokea na kutolea kauli, sasa ukaguzi wa wachimbaji unafanyika kwa staha, nilikuomba kuwekewa kivuli  eneo la kusubiri kukaguliwa uliridhia na kufanyia kazi nakushukuru sana" alikiri Sendeka.


Ameendelea kusema, nchi hii ina mipango tena mipango yenye maono makubwa. Ameeleza kusita kwake kwa maamuzi ya serikali kujenga ukuta wa mirerani na kukiri kuona manufaa yake


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere alisema, Serikali ndio kila kitu kwenye madini ya tanzanite.


Akitoa mfano wa FIFA alisema unapofika wakati wa kutangaza nchi kutakakochezwa mpira kunakuwa hakuna maandalizi yeyote yaliyofanyika na baada ya kupata taarifa hiyo   ndipo huanza maandalizi kwa kujenga viwanja, barabara n.k


"Siasa ikae mbali na mimi, tabia mbaya ikae mbali na mie, maamuzi ya wapi biashara ya tanzanite itafanyika yamefanyika hakuna wa kupinga", alikazia Makongoro.

Comments