Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko (kulia) akisikiliza kwa makini hoja zinazowasilishwa kwake na Mbunge wa jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa tanzanite Mirerani alipokutana nao kusikiliza na kutatua kero zao, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere.
Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Manyara akizungumza wakati wa Mkutano wa Waziri wa Madini na Wachimbaji ndani ya ukuta wa Mirerani

Wananchi wakifuatilia mkutano
Ombi la wafanyabiashara wa tanzanite kusalia na kuuza madini yao popote ulimwenguni limekubaliwa na Serikali kwa sharti la kuhakikisha wanatoka na madini nje ya ukuta baada ya kujaza fomu maalum yenye taarifa ya kiasi cha madini hayo yakiwa yamelipiwa kodi stahiki za Serikali.
Awali walikuwa wakiyarejesha ndani ya ukuta ili kuhifadhiwa baada ya kukosa wanunuzi wa madini hayo jambo ambalo lilikuwa likilalamikiwa na wachimbaji hao kwa kutaka kuyahifadhi wao wenyewe pamoja na kuruhusiwa kusafirisha popote duniani ili kutafuta wateja.
Kibali hicho kimetolewa na Serikali kupitia Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko mwishoni mwa wiki alipofanya kikao na wachimbaji na wafanyabiashara wa tanzanite ndani ya ukuta wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Dkt. Biteko alitoa kibali mara baada ya Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka kuwasilisha ombi hilo pamoja na mengine kwa niaba ya wananchi, wafanyabiashara na wachimbaji wa tanzanite waliopo katika jimbo la Simanjiro.
Aidha, Dkt. Biteko aliwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa tanzanite kushirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara hususani barabara zinazoelekea sehemu zao za machimbo na kueleza kuwa Wizara yake itatafuta namna ya kushiriki katika kuboresha barabara kubwa kama ilivyoombwa na wananchi wa eneo hilo.
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko aliendelea kuwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kupendana na kuacha vitendo vya chuki miongoni mwao ili kuifanya Sekta ya Madini kuendelea kukua na kuongeza mchango wake kwenye uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere aliishukuru Wizara ya Madini na kubainisha kuwa imekuwa msaada sana katika kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka aliwasilisha maombi ya wananchi wa Wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na wachimbaji wa tanzanite kuruhusiwa kujaza fomu maalumu ya madini waliyonayo na kwenda kuyauza nje ya Mirerani tofauti ilivyokuwa ambapo walikuwa wakiwauzia wanunuzi (brokers) waliopo ndani ya ukuta kwa bei ya kutupwa.
Alisema, kufanyiwa kazi kwa ombi hilo kutaondoa ukiritimba kwa baadhi ya wanunuzi wanaonunua tanzanite kwa bei ya kutupwa na hivyo kuwafanya wachimbaji wa tanzanite kunufaika na madini wanayopata.
Pamoja na ombi hilo, Sendeka aliwasilisha ombi la kutengenezewa barabara yenye urefu wa kilomita 5 inayoingia na kutoka nje ya ukuta katika eneo tengefu la mirerani kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za usafiri hususani msimu wa mvua ombi lililoahidiwa kufanyiwa kazi na serikali baada ya kukamilika kwa mchakato wake .
Dkt. Biteko alikuwa na ziara ya siku mbili katika eneo tengefu la Mirerani ambapo alieleza kauli ya Serikali juu ya utekelezaji wa maagizo ya kufanyika kwa biashara ya tanzanite katika mji huo wa Mirerani mkoani Manyara.
Comments
Post a Comment