TANCOAL WAKUMBUSHWA KULIPA DENI LA SERIKALI





Waziri wa Madini, Doto Biteko, ameitaka Kampuni ya uchimbaji Makaa ya Mawe ya TANCOAL kuanza kulipa deni inalodaiwa na Serikali.


Waziri Biteko ametoa maagizo hayo alipotembelea mgodi huo  unaozalisha Makaa ya Mawe  unaomilikiwa na Kampuni ya TANCOAL wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma.


Kampuni ya Tancoal iliyoanza rasmi uzalishaji mwaka 2011 inawafanyakazi zaidi ya 110.


Imeelezwa kuwa, Kampuni hiyo inadaiwa na Serikali kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kodi mbalimbali za Serikali.


Akizungumza na uongozi wa Kampuni hiyo, Waziri Biteko ameitaka Kampuni hiyo kuanza kulipa deni hilo kwa awamu katika Mwaka huu wa Fedha 2021/2022.


“Lile deni mnalodaiwa na Selikali nataka kuona mwezi huu mnaanza kulilipa, hatutaki mfirisike, tunataka watanzania waendelee kuwa na  ajira, jitahidini mtupe ratiba hata ya muda mrefu lakini muanze kulipa mwezi huu,” amesema Waziri Biteko.


Aidha, Waziri Biteko ameitaka Kampuni hiyo kutekeleza Sheria ya Kuchangia Maendeleo kwa Jamii (CSR) baada ya kugundua hawatekelezi matakwa ya Sheria hiyo.


Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amesema katika suala la uchangiaji huduma kwa jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ndio inapaswa kupanga miradi itakayotekelezwa katika mwaka husika na kuwasilisha kwa Kampuni ya TANCOAL kwa ajili ya utekelezaji.


“haiwezekani Kampuni itekeleze Sheria ya Uchangiaji Huduma kwa Jamii bila kuishirikisha Halmashauli husika, kila Halmashauri ina vipaumbele vyake ambavyo imepanga kuvitekeleza kupitia mchango wa CSR, hivyo lazima mkae na Halmashauri ili mjue vipaumbele vya Halmashauri ya wilaya,” amesema Prof. Msanjila.


Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Kampuni ya TANCOAL, Bosco Mabena amesema, Kampuni hiyo inakabiliwa na changamoto ya masoko changamoto ya kushuka bei ya Makaa ya Mawe.


Pia, Mabena amesema kuwa, kipindi hiki uchimbaji wa Makaa ya Mawe umekuwa mgumu kwa sababu Makaa hayo yemeenda chini zaidi hivyo kupelekea gharama za uzalishaji kuongezeka.

Comments