Rais Samia amezindua Kiwanda cha kisasa cha kusafisha Dhahabu





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Juni 13, 2021 amezindua kiwanda cha kisasa cha kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery Ltd kilichopo jijini Mwanza. 


Akihutubia wananchi wa Mwanza mara baada ya kuzindua kiwanda hicho, Rais Samia amebainisha faida lukuki za kiuchumi zitakazotokana na uongezaji thamani madini, ikiwemo kuhamasisha uwekezaji mkubwa nchini na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha madini ya Tanzania yanaongezwa thamani hapa nchini kama Sheria ya Madini Sura ya 123 inavyoeleza. 


Kutokana na uwekezaji huo, Rais Samia amelipongeza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na wabia wqenza Kampuni za Rozella General Trading LLC ya Dubai na Kampuni ya ACME Consultant Engineering Pte Ltd ya nchini Singapore kwa ujenzi kiwanda hicho cha kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na moja ya viwanda vikubwa barani Afrika ambacho kinatarajia kuchochea shughuli za uongezaji thamani nchini.


Rais Samia ameyataja manufaa mengine yanayotokana na shughuli za uongezaji thamani madini kuwa ni pamoja na kuongeza mapato ya serikali na kukuza soko la ajira kupitia Sekta ya Madini.


Akizungumzia faida za kiwanda hicho, Rais Samia amesema kuwa ni pamoja na serikali kupata mapato kupitia mrabaha, ada na tozo.

“Faida nyingine za mradi zinahusisha ajira mpya za moja kwa moja zipatazo 120  na  ajira 400 zisizo za moja kwa moja  pamoja na watanzania kupata ujuzi wa teknolojia mpya za kisasa za kusafisha dhahabu," amesema Samia.


Pia, Rais  Samia ameongeza kwamba, kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba hisa za STAMICO zitakuwa zikiongeza kwa asilimia 5 kufikia 51.

Vilevile, amesema kwamba, kiwanda hicho kitawezesha kubaini madini ambata na kuweza kujua thamani yake suala ambalo litaisaidia serikali kukokotoa mapato stahili kwa madini hayo. 


Ameongeza kuwa, kufuatia dhahabu hiyo kusafishwa kwa viwango vya kimataifa  Tanzania inaingia kwenye medani za nchi ambazo zinasafisha dhahabu na hivyo Benki Kuu ya Tanzania itaweza kunua dhahabu hiyo na kuiweka kama amana na hivyo kuiwezesha Serikali kukusanya mrabaha kwa kuchukua dhahabu badala ya fedha.


“Pamoja na mafanikio ambayo STAMICO imepata, bado nawataka waongeze juhudi zaidi katika kuendeleza Shirika lifikie maendeleo ya juu. Kwa upande wa Serikali, itaendelea kuliimarisha Shirika hili ili liweze kushiriki katika shughuli za madini kwa tija zaidi na kwa manufaa ya umma.


Akizungumzia mipango ya Serikali katika kuiimarisha Sekta ya Madini, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuyasimamia masoko yaliyoanzishwa maeneo mbalimbali nchini na kuyaboresha ili kuhakikisha madini yanayongezwa thamani nchini, ikiwemo kuimarisha mgodi wa madini ya tanzanite ambayo unaihitaji kutangazwa kikamilifu kutokana na upekee wake  na kuwekewa mfumo wa kuyadhibiti.


Vilevile,  ameitaka Wizara ya  Madini kuendelea  kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kuchimba kwa tija jambo ambalo ameeleza kuwa, litasaidia kuongeza uzalishaji ikiwemo madini ya dhahabu ambayo ni malighafi ya kiwanda hicho.


Naye, Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza katika uzinduzi huo amesema kuwa, matokeo ya uanzishwaji wa kiwanda yametokana na mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2017 ambayo imesisitiza shughuli za uongezaji thamani kufanyika nchini ikiwemo kubainisha msimamizi Mkuu wa rasilimali Madini kuwa Ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mbali  na kiwanda hicho, Waziri Biteko ameieleza hadhira iliyohudhuria uzinduzi huo  kuhusu uwepo wa  viwanda vingine viwili vya kusafisha dhahabu ambavyo viko katika mikoa ya Geita na Dodoma  na kueleza kuwa, kiwanda cha Geita kina uwezo wa kusafisha kilo 450 kwa siku na cha Dodoma kina uwezo wa kusafisha kilo 30 kwa siku.


Kufuatia Uzinduzi huo Waziri Biteko ameainisha mapato ambayo Serikali itapata kufuatia mwenendo mzuri wa uzalishaji kama matarajio ya kiwanda na kueleza kwamba serikali itapata shilingi bilioni 744 kwa Mwaka, Halmashauri shilingi bilioni 36 kwa Mwaka na STAMICO itapata shilingi bilioni 21 kwa mwaka.


Kuhusu mwenendo  wa Sekta ya Madini  Waziri Biteko amesema kuwa mchango wa Sekta umekua kufikia asilimia 6.7 Mwaka 2020 kutoka asilimia 4.5 mwaka 2015.


" Mhe. Rais hadi kufikia tarehe 1 Juni Wizara imekusanya shilingi bilioni 544 na kuvuka kutoka  shilingi bilioni 526 tulizopangiwa kukusanya mwaka huu wa fedha," amesema Biteko.


Akizungumzia mapinduzi makubwa yaliyofanywa na STAMICO amesema kuwa Shirika hilo kwa sasa linafanya kazi vizuri na kuweza kujiendesha lenyewe kwa kutumia mapato yake ya ndani.


“Kwa mara ya kwanza  tangu kupata uhuru, Tanzania inaweka historia ya kuwa miongoni mwa nchi zinazosafisha madini yake,” alisisitiza Waziri Biteko.


Akitoa taarifa ya mradi wa kiwanda hicho katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amesema kuwa kiwanda hicho ni matokeo ya Mabadiliko ya Sheria ya Madini Mwaka 2017 yakihamasisha uongezaji thamani wa madini nchini.


Aidha, Prof. Msanjila amefafanua kuhusu  mradi huo na kusema kuwa,  umegawanyika katiika miradi midogo mitatu ukihusisha  ujenzi wa miundombinu ya majengo na mitambo ambapo itahusisha Soko la Madini. Ameitaja miradi mingine kuwa ni pamoja kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata mitaji na vifaa na wa tatu ni mradi wa kuuza na kununua dhahabu.

  

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Mwanza Precious Metal Refinery Bw. Anand Mohan ameishukuru serikali ya tanzania kwa kumpa ushirikiano katika uwekezaji wake tangu kuanza kwake.


Ameiomba Serikali kuzuia usafirishwaji wa madini ghafi ili kukiwezesha kiwanda hicho kupata malighafi za kutosha.

Kiwanda cha kusafisha Dhahabu cha Mwanza  kina uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa kiwango cha Kimataifa kwa ubora wa asilimia 999.9 purity . Aidha kiwanda hicho kimewekewa Uwekezakano wa kusafisha hadi kilo 960 kwa siku.

Kiwanda hicho kimegharimu kiasi  cha Dola za Marekani milioni 5.2 sawa na takriban shilingi bilioni 12.2 .

Kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza  kina uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa kiwango cha Kimataifa kwa ubora wa asilimia 999.9 purity. Aidha, kiwanda kimewekewa uwezekano wa kusafisha hadi kilo 960 kwa siku.

Comments