DC NKUMBA ATOA SIKU 14 UKARABATI MACHINJIO YA KATENTE.


Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Mhe.Said Nkumba ametoa siku 14  kuhakikisha  Machinjio ya Katente inakarabatiwa na kuanza kufanya kazi ili wananchi waweze kupata huduma ya machinjio na nyama katika mazingira mazuri.


Maelekezo hayo ameyatoa leo tarehe 14 Juni, 2021 akiwa na Viongonzi wa halmashauri ya Wilaya ya Bukombe pamoja na Wataalamu baada ya Kamati ya Siasa  Mkoa kufunga kwa muda machinjio ya Mwalo tarehe 10 Juni, 2021 wakati wa ziara katika halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.


"Machinjio ya Mwalo ipo bondeni hivyo wakati wa mvua mazingira yake kuyaweka katika hali ya usafi si shughuli nyepesi hivyo basi kwa kuwa halmashauri ilikwishajenga machinjio nyingine katika eneo la Katente  hivyo basi natoa maelekezo kwa halmashauri kuhakikisha ndani ya siku 14 Machinjio ya Katente inafanyiwa malekebisho ili kuhamisha kabisa eneo la Mwalo lisitumike tena kama machinjio."


Aidha Nkumba ametoa maagizo kwa Meneja wa TANESCO Wilaya, Meneja wa RUWASA pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Maji Mjini Ushirombo kuhakikisha huduma ya Umeme na maji inapatikana katika Machinjio mpya ya Katente.


Naye Mwenyekiti wa halmashauri Wilaya ya Bukombe Mhe. Yusuph Mohamedi Yusuph Diwani wa kata ya Bulangwa amesema "Tumeanza utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya Siasa Mkoa Chama Cha Mapindunzi kama tulivyoahidi"


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe Dionis Myinga amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Bukombe kuyafanyia kazi maagizo  yaliyotolewa.


"Maelekezo uliyoyatoa tumeyapokea, tunakwenda kuyafanyia kazi na tutahakikisha tunasimamia kikamilifu masuala ya usafi katika machinjiyo hiyo mpya kwa ajili ya afya za wananchi wetu"


Kwa upande wake Afisa Mifugo Msaidizi Kata ya Mwalo Allyson Kinyunyu amesema Machinjio ya Mwalo inachinja ng'ombe 5 mpaka 6 kwa siku na halmashauri inapata mapato kiasi cha shilingi laki 7 hadi 8 kwa mwezi na shilingi Milioni 8 hadi 9 kwa Mwaka na siyo Milioni 300 kwa mwaka kama ilivyoelezwa  kwenye ziara ya kamati ya Siasa Mkoa.

Comments