WAZIRI BITEKO ATOA MWONGOZO UREJESHWAJI WA MADINI KAMPUNI YA TANZANITE AFRIKA



Waziri wa Madini Doto Biteko leo tarehe 27 Aprili, 2021 amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanzanite Afrika Wilfredy Mushi pamoja na Viongozi wengine jijini Dodoma ajenda ikiwa ni Kampuni ya Tanzanite Afrika kuiomba Serikali kurejesha madini ya kampuni hiyo yaliyohifadhiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mwaka 2017.


Waziri Biteko amekutana na Kampuni hiyo ikiwa ni sehemu ya kutatua kero ya Tanzanite Afrika baada ya Madini yao kuchukuliwa Mwaka 2017 hatua iliyopelekea Serikali kuchukua madini hayo na kwenda kuyahifadhi BoT baada ya mnunuzi kukosekana kwenye mnada huo uliyofanyika Mirerani.


"Naelekeza Uongozi wa Kampuni ya Tanzanite Afrika kupeleka maombi maalumu kwa Wizara ya Madini ili Majadiliano yafanyike kuhusu urejeshaji wa madini hayo kutoka BoT" amesema Waziri Biteko.


Waziri Biteko amesema barua hiyo iandaliwe kwa kuainisha vitu vyote muhimu ili taratibu zifanyike na madini yarejeshwe na kuuzwa.



Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya amemueleza Waziri Biteko kuwa, Madini hayo yalipelekwa BoT ikiwa ni moja ya hatua ya kuyahifadhi hadi pale utaratibu wa kuyarejesha utakapopangwa na Serikali.



 Prof. Manya ametumia nafasi hiyo pia kuwaelekeza kufuata maelekezo waliyopewa na Waziri Biteko kwa kupeleka maombi maalumu ili timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini waandae utaratibu utakaofaa ili kurejesha madini hayo na Serikali ikusanye kodi.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzanite Afrika Wilfredy Mushi amemueleza Waziri Biteko kuwa, Kampuni yao imekuwa ikifuatilia madini hayo yenye thamani ya Dola za Marekani Laki 4 kuanzia Mwaka 2017 ikiwa ni baada ya Serikali kuyahifadhi BoT, ikiwa ni hatua iliyofikiwa na pande za wauzaji na Serikali baada ya wanunuzi kukosekana wa madini hayo.



Mwinyi amemuhakikishia Waziri Biteko kuwa wapo tayari kufuata maelekezo ya Serikali ikiwa ni pamoja na kulipia mrabaha ili madini hayo yarejeshwe na kuuzwa tena.

 

Katika hatua nyingine Waziri Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Benki ya UBA ( United Bank of Afrika) wenye lengo la kujadili fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini.


Waziri Biteko ameueleza uongozi wa benki hiyo kuwa, kuna fursa nyingi za uwekezaji kwenye Sekta ya Madini huku akisisitiza UBA kuwekeza zaidi kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wafanyazi wa wizara. 


Waziri Biteko amesisitiza UBA kutumia makongamano mbalimbali yanayoandaliwa na Wizara ya Madini ili waweze kujitangaza zaidi na kutambulika na kuifanya Sekta hii ya madini kuwa na tija kwa Taifa.

Comments