WAZIRI BITEKO AFUNGUA MKUTANO WA SABA WA MAWAZIRI

 

 

Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma kuhusu taarifa ya mkutano wa 7 wa Mawaziri wa nchi za Afrika zinazozalisha madini ya Almasi, unaoanza leo tarehe 7 Aprili 2021 mpaka tarehe 8 Aprili 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal)
Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko akiteta jambo na Naibu Waziri wa Madini Mhe Prof Shukrani Manya wakati wa mkutano na Waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma kuhusu taarifa ya mkutano wa 7 wa Mawaziri wa nchi za Afrika zinazozalisha madini ya Almasi, unaoanza leo tarehe 7 Aprili 2021 mpaka tarehe 8 Aprili 2021.


Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko (Mb) amefungua mkutano wa 7 wa Mawaziri wa nchi za Afrika zinazozalisha madini ya Almasi (AFRICAN DIAMONDS PRODUCERS ASSOCIASION-ADPA) unaoanza leo tarehe 7 Aprili 2021 hadi tarehe 8 Aprili 2021 Kwa njia ya Mtandao (Video Conference).

Katika mkutano huo wa nchi wananchama wazalishaji wa Almasi, Tanzania ndio nchi mwenyeji wa mkutano huo ikipokea kijiti cha uenyekiti wa jumuiya hiyo kutoka nchi ya Jamhuri ya Namibia ambayo inamaliza muda wake kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Biteko amesema kuwa Mkutano huo wa siku mbili utahusisha ushiriki wa mawaziri na wataalamu wa madini kutoka nchi 12 wanachama kujadili maswala mbalimbali katika sekta ya madini.

Mhe Biteko amezitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini, Namibia, Tanzania, Zimbabwe, Cameroon, Afrika ya Kati, Ghana, Togo, Guinea, na Seera Leone.

Aidha, katika mkutano huo kutakuwa na nchi saba waangalizi ambazo ni Algeria, Jamhuri ya Congo, Ivory Coast, Gabon, Liberia, Mali na Mauritania.

Waziri Biteko amebainisha hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma na kuongeza kuwa mkutano huo unaotarajia kufanyika leo tarehe 7 Aprili 2021 utajadili maswala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya ADPA na mkutano wa tarehe 8 Aprili 2021 wa Mawaziri utahusika kutoa maamuzi ya maswala hayo pia.

Pamoja na mambo mengine Tanzania itapata fursa ya kubadilishana uzoefu na nchi wanachama kuhusiana na usimamizi wa sekta ya madini na kuimarisha utendaji katika wizara ya madini

Waziri Biteko amesema kuwa katika kipindi chote cha uenyekiti serikali ya Tanzania itahakikisha kuwa inaboresha mifumo ya jumuiya ya ADPA ili iweze kuwa na manufaa kwa nchi wanachama

Comments