MKUTANO WA ADPA WAMALIZIKA JIJINI DODOMA, ZIMBABWE MAKAMU MWENYEKITI-MHE BITEKO

 

Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa 7 wa Mawaziri wa nchi za Afrika zinazozalisha madini ya Almasi uliofanyika kwa njia ya Mtandao (Video Conference) leo tarehe 8 Aprili 2021.


 

Mawaziri wanaounda Umoja wa nchi za Afrika zinazozalisha madini ya Almasi (AFRICAN DIAMONDS PRODUCERS ASSOCIASION-ADPA) kwa kauli moja wameridhia Lugha ya Kiswahili kutumika katika mikutano ya ADPA.

 

Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko (Mb) amebainisha hayo wakati wa mkutano wa 7 wa Mawaziri wa nchi za Afrika zinazozalisha madini ya Almasi ambao umefanyika Jijini Dodoma leo tarehe 8 Aprili 2021 kwa njia ya Mtandao (Video Conference).

 

Makubaliano hayo yamepelekea Lugha ya Kiswahili kupenya katika mkutano huo hivyo Mkutano maalumu wa ADPA kuwa na lugha 4 ambazo ni Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili pamoja na Kireno.

 

Katika mkutano huo wa nchi wananchama wazalishaji wa Almasi, Tanzania ndio nchi mwenyeji wa mkutano huo ikipokea kijiti cha uenyekiti wa jumuiya hiyo kutoka nchi ya Jamhuri ya Namibia ambayo inamaliza muda wake kwa kipindi cha mwaka mmoja.

 

Pia Mawaziri hao wamekubaliana nchi ya Zimbabwe kuwa Makamu mwenyekiti wa ADPA katika kipindi cha miaka miwili.

 

Waziri Biteko amesema kuwa mara baada ya kipindi cha uenyekiti kwa Tanzania kumalizika nchi ya Zimbabwe itashika nafasi hiyo.

 

Kadhalika, Mawaziri hao wamekubaliana kuwa Kamati tendaji ya ADPA kupitia upya mfumo wa kimenejimenti ili kuweza kuona eneo gani sahihi kwa ajili ya maboresho.

 

Biteko amesema kuwa Mkutano huo wa siku mbili ulioanza jana tarehe 7 Aprili 2021 na kufikia ukomo tarehe 8 Aprili 2021 umehusisha ushiriki wa mawaziri na wataalamu wa madini kutoka nchi 12 wanachama kujadili maswala mbalimbali katika sekta ya madini.

 

Mhe Biteko amezitaja nchi wanachama wa mkutano huo kuwa ni pamoja na Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini, Namibia, Tanzania, Zimbabwe, Cameroon, Afrika ya Kati, Ghana, Togo, Guinea, na Seera Leone

Comments