MAJARIBIO YA AWALI KIWANDA CHA KUSAFISHA DHAHABU MWANZA YAONESHA MATOKEO MAZURI



Imeelezwa kuwa, Majaribio ya Awali ya Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metal Refinery ambacho ni Ubia kati ya Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO.), yameonesha Matokeo Mazuri.

 


Katika mradi huo, STAMICO ina ubia wa asilimia 25 na kampuni za Rozella General Trading LLC ya Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) pamoja na Kampuni ya ACME Consultant Engineers PTE Ltd ya Singapore zina ubia wa asilimia 75. 


Waziri Biteko ameeleza kuwa, kukamilika kwa kiwanda hicho pamoja na viwanda vingine vya Eyes of Africa Ltd kilichojengwa  jijini Dodoma na Geita Gold Refinery cha Mkoani Geita, ni mapinduzi mengine ya kiuchumi kwa Tanzania kupitia Sekta ya Madini kwa kuwa taifa sasa linakwenda kusafisha madini yake hapa nchini.


Vilevile, ameongeza kuwa, Kiwanda cha Mwanza Precious Metals Refinery kinatarajia kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku, huku kiwanda cha Geita kikiwa na uwezo wa kusafisha dhahabu kiasi cha nusu tani kwa siku na kiwanda cha  Eyes of Africa  cha Dodoma kina uwezo wa kusafisha dhahabu kilo 50 kwa siku.


Waziri Biteko ameainisha kuwa, mbali ya viwanda hivyo kuiwezesha serikali kupata mapato kupitia tozo na mrabaha pia, vinatarajiwa kuleta teknolojia za kisasa nchini, ikiwemo kutoa ajira kwa watanzania na kuongeza kuwa, ‘’kwa upande wa kiwanda cha Mwanza, katika utekelezaji wake wa  awali, kinatarajiwa kutoa ajira zipatazo 100’’.


Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse, aliieleza kamati hiyo kuwa,kutokana na kuwa na teknolojia ya kisasa, kiwanda hicho kina uwezo wa kusafisha dhahabu hadi asilimia 999.9 (purity) ya ubora ambao ni wa kiwango cha kimataifa kinachoweza kununuliwa na Benki Kuu popote duniania kwa ajili ya kuhifadhiwa.


Pia, Dkt. Mwasse aliieleza Kamati hiyo kuwa, mitambo ya kiwanda  hicho imewekewa uwezekano wa kuongeza uzalishaji  zaidi hadi kilo 960 kwa siku.


Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara, kiwanda hicho kinarajia kuanza uzalishaji ifikapo tarehe 20 Aprili, mwaka huu.


Comments