Stamico yakamilisha kiwanda cha Dhahabu Mwanza

 

Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) kwa kushirikiana na kampuni ya Rozella General Trading kutoka nchini Dubai limekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kusafisha dhahabu jijini Mwanza (Mwanza Precious Metal Refinery) kwa ubora wa kimataifa hadi kufikia asilimia 999.99.

Akitoa taarifa Februari 15, 2021 kwa Waziri wa Madini Doto Biteko aliyetembelea ujenzi wa kiwanda hicho ili kujionea maendeleo ya ufungaji mitambo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa shirika hilo Dkt. Venance Mwasse alisema kukamilika kwake kunatoa fursa ya biashara ya madini kufanyikia hapa nchini badala ya kusafirisha madini ghafi kwenda nje ya nchi na hivyo kulikosesha Taifa mapato.

Dkt. Mwase alisema hadi sasa ujenzi wa kiwanda hicho ambacho kiko mbioni kuanza kazi mwezi Machi 2021 umegharimu shilingi za kitanzania bilioni 8.9 na kwamba kitakuwa na uwezo wa kusafisha kilo 480 kwa siku na kukuza mapato ya Serikali kupitia Wizara ya Madini hadi kufikia shilingi bilioni 600 kwa mwaka pamoja na ajira za kudumu 120 kwa watanzania.

Akizungumza baada ya kukagua kiwanda hicho ambacho ujenzi wake ulianza mwezi Machi 2020, Waziri wa Madini Doto Biteko alisema ni kiwanda cha kwanza kujengwa nchini na cha tatu barani Afrika na kwamba kitawezesha wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika na thamani halisi ya fedha baada ya kuuza dhahabu yao ikiwa imesafishwa.

Aidha Biteko alitumia fursa hiyo kuwahimiza wachimbaji wadogo nchini wasikubali kuuza dhahabu yao nje ya nchi kabla ya kusafishwa kwenye kiwanda hicho pindi kitakapoanza kufanya kazi huku pia akitoa muda wa wiki mbili kwa STAMICO kuhakikisha wanaanza kununua dhahabu kwa wachimbaji wadogo.

Naye Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella aliipongeza Wizara ya Madini na taasisi zake ikiwemo Tume ya Madini pamoja na STAMICO kwa kushirikiana vyema na mwekezaji kujenga kiwanda hicho ambacho kitakuza thamani ya raslimali za madini nchini tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo yalikuwa yakisafirishwa kama madini ghafi na kwamba matarajio ni kuhakikisha ulinzi unaimaishwa kiwandani hapo na kutoa tija kwa watanzania.

Ujenzi wa kiwanda hicho ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambayo amekuwa akiyatoa kwa Wizara ya Madini kuhakikisha raslimali zilizopo zinalinufaisha Taifa badala ya kuchimbwa na kusafirishwa kwenda nje ya nchi kama malighafi.

Waziri wa Madini, Doto Biteko (mwenye tai) akiwa na viongozi mbalimbali alipotembelea kiwanda cha kusafisha dhahabu jijini Mwanza. Kushoto ni mwakilishi wa kampuni ya Rozella General Trading, Ananel Mohan Mahajan na kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya pamoja ya ujenzi wa kiwanda hicho, Deusdedith Magala.
Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati) Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof Simon Msanjila (wa tatu kushoto), Mkuu wa Mkoa Mwanza John Mongella (mwenye kofia nyeusi) pamoja na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye ziara hiyo.
Hatua ya ujenzi wa kiwanda cha kusafisha dhahabu jijini Mwanza pia inatoa fursa kwa nchi jirani kuleta dhahabu yake hapa nchini kwa ajili ya kusafishwa. Pia STAMICO inajiandaa kuwawezesha wachimaji wadogo ili kuchimba kwa tija na kupata madini/ dhahabu kwa ajili ya uendeshaji wa kiwanda hicho.
Kaimu Mtendaji Mkuu STAMICO, Dkt. Venance Mwasse (kulia) akitoa ufafanuzi wa kiwanda hicho kwa Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati). Kushoto ni Mkuu wa Mkoa Mwanza John Mongella.

Comments