BITEKO: 2025 SEKTA YA MADINI KUCHANGIA 10% KATIKA PATO LA TAIFA



Imeelezwa kuwa, ifikapo mwaka 2025 Sekta ya Madini inatakiwa iwe imefikia lengo la kuchangia asilimia 10% ya mchango wake kwenye Pato la Taifa. 


Hayo yamebainishwa na Waziri Biteko leo Februari 03, 2021 alipofanya kikao na Watumishi wa Tume ya Madini kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) jijini Dodoma.


Waziri Biteko amesema, Sekta ya Madini imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka na sasa ndio sekta inayoongoza kwa kuingizia nchi fedha za kigeni na kuongeza kuwa sekta hiyo imekua kwa asilimia 17.7 mwaka 2019 na kuongoza katika ukuaji ukilinganisha na sekta zingine hapa nchini ambapo mchango wake umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019.


“Pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika Sekta ya Madini lakini bado tuna kazi ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 sekta hii inatoa mchango wa asilimia 10% katika Pato la Taifa, hivyo niwaombe watumishi wote wa Tume ya Madini kuongeza bidii na kuachana na tamaa ambazo zitatufanya tusifikie malengo yetu,” amesema Waziri Biteko.


Waziri Biteko aliongeza kuwa, mwaka 2020/2021 Wizara ya Madini imepewa kadirio la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 526, lakini Wizara imejiwekea lengo la kuhakikisha baada ya miaka 4 iliyobaki kufikia 2025 inafikia lengo la kuchangia asilimia 10% katika pato la Taifa ambapo amewasisitiza watumishi wote wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kwamba hiyo kazi ni ya kila mmoja.


Pia, Waziri Biteko amechukizwa na watumishi wasio waaminifu ambapo ameeleza kuwa wale watakaokwamisha juhudi za Wizara kwa namna yoyote ikiwemo tamaa, hao wanachafua Wizara na hawatakuwa na nafasi ya kufanya kazi katika Wizara ya Madini wala kwenye Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.



Katika hatua nyingine, Waziri Biteko amewataka Watumishi wa Tume ya Madini kupendana na kuachana na majungu, fitina na badala yake wafanye kazi kwa kushirikiana na kueleza kuwa Tume ya Madini ndio Moyo wa Wizara ya Madini na ndiyo chombo muhimu kinacho mshauri Waziri katika mambo ya Sera na Sheria za Madini.


Awali, Mwanyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amesema, Tume ya Madini inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa ofisi, hivyo Serikali imetoa bilioni 4.6 kwa ajili ya kujenga jengo la Tume ya Madini na Mkandarasi yupo katika eneo la ujenzi kwa hatua za mwanzo.


“Tunaipongeza Serikali kwa kusikia kilio chetu cha upungufu wa ofisi tunashukuru Mkandarasi ameshasafisha eneo na mwishoni mwa wiki hii ataanza ujenzi wa msingi ambapo ametuahidi atamaliza ujenzi ndani ya miezi 8,” amesema Prof. Kikula.



Naye, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amemuomba Waziri Biteko kuwapa nafasi za kudumu Watumishi wanao kaimu nafasi walizonazo kwa muda mrefu hususan Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.


Wakati huo huo, Mhandisi Samamba amemuomba Waziri Biteko kuangalia upya maslahi ya Watumishi ambapo amesema wengi wanalalamika kutorekebishiwa maslahi yao hata baada ya kupanda madaraja.

Comments