AKATAA KUONGEZWA LANGO LA PILI, MGODI UTAKAOHUSISHWA NA UTOROSHAJI KUFUTIWA LESENI, AAGIZA MAENEO YA UKAGUZI KUONGEZWA, PROF. MANYA ASEMA WANATAMANI TANZANITE KUWA NEMBO YA TANZANIA
Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema Serikali haitaongeza Lango la Pili katika Ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani bali itaendelea kuwa na lango moja tu la kuingilia kama ilivyo sasa kutokana tabia ya baadhi ya wadau katika eneo hilo kuendeleza vitendo vya kutorosha madini ya Tanzanite.

Waziri Biteko amesisitiza kwa sasa serikali haiwezi kuongeza lango hilo mpaka hapo baadaye itakapoona ipo haja ya kufanya hivyo baada ya kufanya utafiti wa kina na kujiridhisha kwamba, hakuna vitendo vyovyote vinavyotokea vya utoroshaji wa Tanzanite.

Kufuatia malalamiko hayo, Waziri Biteko amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini kuwasiliana haraka na Kampuni ya SUMA JKT ili kuanza haraka kwa ujenzi huo.

Kufuatia kauli hiyo, Waziri Biteko amemwagiza Afisa Madini Mkazi Mirerani kuwaandikia barua wasimamizi wote wa migodi iliyopo ndani ya ukuta ili kufahamishwa kuhusu suala hilo.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko ametoa ruksa kwa wachimbaji katika eneo hilo kupata huduma ya baruti kutoka kwa kampuni yoyote isipokuwa tu iwe na uhalali wa kufanya shughuli hizo ka mujibu wa Sheria.

Akijibu kuhusu suala la TAMIDA kupatiwa sehemu ya kufanya biashara badala ya kutembea umbali mrefu kwenda jijini Arusha, Waziri Biteko amewashauri wadau hao kutafuta eneo kwa ajili ya kazi hiyo na serikali kupitia wizara italiidhinisha kwa mujibu wa sheria na kusititiza kuwa, sehemu ya kufanya Arusha itabaki kuendelea kuwa Soko la Kimataifa.

Amesema kuwa, serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya usalama ikiwemo miundombinu ya barabara ndani ya eneo linalozunguka migodi ya tanzanite na kuongeza kwamba, tayari serikali imekwishaanza kulifanyia kazi suala hilo. Naibu Waziri Manya amelielezea suala la barabra ndani ya ukuta baada ya Mbunge wa Simanjiro kulieleza kama changamoto kwa wadau ambayo serikali inapaswa kuifanyia kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti amewataka wadau wa madini mkoani humo kutumia mamlaka kwa kufuata ngazi za kiutendaji pindi wanapotafuta nafasi ya kutatuliwa kero zao.

Kauli ya Mkuu wa Mkoa imekuja kufuata ombi lililowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara wa Madini Nchini (TAMIDA), Sam Mollel ambaye amelalamikia kuwepo kwa hali ya kutozwa kodi ya pango katika Soko la Madini ambalo wameiomba iondolewe ikiwemo changamoto kadhaa kati ya wadau hao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambapo ameeleza kuwa, kutatuliwa kwa changamoto zinazowakabili kutapelekea kuwawezesha wadau hao kupata hamasa ya kuendelea kufanya shughuli zao vizuri na hivyo kuchangia zaidi katika sekta husika.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Zephania Chaula amesisitiza ukaguzi wa kina kuendelea kufanyika katika eneo hilo kutokana na wadau kutoheshimu taratibu kwa kuendeleza na tabia za kutorosha madini ya tanzanite.
‘’Ukitaka uheshimiwe, tuheshimu. Kama kusingekuwa na tabia ya kudokoa hata askari tusingewaweka hapa, lakini kwa tabia hii inayofanyika, ukaguzi uko pale pale,"amesisitiza Mhandisi Chaula.
Kauli ya Mhandisi Chaula inafuattia wadau hao kuwasilisha kero kuhusu ukaguzi wa kina unaofanywa eneo hilo.
Mkutano huo kati ya Waziri wa Madini uliomshirikisha pia Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya, Uongozi wa Mkoa wa Manyara, Watendaji wa Wizara, Tume ya Madini na wadau wa madini mkoani humo, umelenga kusikiliza na kutatua kero mbalimbali katika eneo la Mirerani.
Comments
Post a Comment