Asisitiza
Utekelezaji wa Yaliyoanishwa kwenye Ilani ya CCM
Ataka Ubunifu kuwezesha Uwekezaji Mkubwa
Ataka Kuhuishwa Sera ya Madini ya Mwaka 2009
Azuia Urasimu usio na Sababu
Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake wamekumbushwa kuzingatia
maeneo muhimu ya kipaumbele yanayopaswa kutekelezwa kwenye Sekta ya
Madini kama yalivyoanishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ya Mwaka 2020-2025, Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Magufuli aliyoisoma wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri
ya Muungano Novemba, 2020 na Hotuba aliyoitoa Bungeni Mwaka 2015.
Hayo yamebainishwa Desemba10, 2020 na Waziri wa Madini Doto Biteko katika
kikao chake na Menejimenti ya Wizara na taasisi zake, baada ya kuteuliwa na
kuapishwa tena kuiongoza Wizara ya Madini.
Biteko amewataka viongozi hao kurejea tena maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ya Mwaka 2015 -2020 ili kuona ni namna gani masuala hayo
yametekelezwa huku kila taasisi ikitakiwa kuhakikisha inayafanyia kazi
maelekezo yote kwa lengo la kuhakikisha Sekta ya Madini inazidi kukua na
kuongeza tija kwa taifa ikizingatiwa kuwa, hivi sasa sekta hiyo imeonekana kuwa
kichocheo cha ukuaji kwa sekta nyingine kiuchumi.
Aidha, Waziri Biteko amesisitiza suala la ubinifu ili kuwezesha kuibuliwa kwa
miradi mikubwa ambayo itapelekea kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka nje ya
Tanzania na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye maendeleo na
uchumi wa nchi.
Kadhalika, Waziri Biteko amezuia urasimu katika kushughulikia masualayanayohusu sekta ya madini akilenga kuweka mazingira bora yatakayowezesha
biashara ya madini kufanyika kwa ufanisi ili kuwezesha matokeo chanya katika
ukusanyaji wa mapato ya serikali ikiwemo kuwezesha uwekezaji katika sekta ya
madini kufanyika bila kuwepo vikwazo visivyokuwa na sababu.
‘’ Kama kuna watu wanataka kuchimba wapewe lesni na wapewe fursa na kama
kuna maoni yanayohusisha taasisi nyingine basi yafanyiwe kazi haraka. Tuwalee
wawekezaji tulio nao ili waendelee kufanyakazi,’’ amesisitiza Biteko.
Ametaka kuwepo kwa mazingira wezeshi yatakayopelekea wafanyabishara na
wachimbaji kufanya shughuli zaokwa amani ili kuwezesha kuzalishwa kwa ajira,
teknolojia mpya za uchimbaji na uchenjuaji wa madini vilevile, kuiwezesha sekta
kuzalisha mabilionea wengi.
Vilevile, Waziri Biteko ametaka kufanyiwa kazi suala la utoroshaji wa madini ili
kuzuia mianya inayopelekea kutoroshwa kwa madini ambalo ameeleza awali
lilianza kufanyiwa kazi vizuri lakini kwa sasa tabia hiyo imeanza kurejea.
‘’ Mwanzo tulikwenda vizuri lakini sasa tabia hii imeanza kujirudia. Kwenye
upande madini feki tumepambana nao na tumekamata mitandao ya watu wa
madini feki,’’ amesema Biteko.
Katika hatua nyingine, Waziri Biteko ametaka kuhuishwa kwa Sera ya Madini ya
Mwaka 2009 ili iendane na matakwa ya sasa akirejea Marekebisho yaliyofanyika
katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.
‘’ Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ni ya muda mrefu. Sera hii ianze kuhuishwa
haraka ili iandane na matakwa ya sasa kama tulivyofanya kwenye Sheria ya
madini ambayo ilitoa nafasi ya kurudisha umiliki wa madini kwa wananchi,’’
amesema Waziri Biteko.
Pia, ametaka suala la kuanzishwa kwa Chama Cha Wajiolojia kupewa msukumo
ili likamilishwe haraka ili kuongeza uwajibikaji wa Wataalam hao katika sekta ya
madini.
Aidha, katika kikao hicho, Waziri Biteko ametumia fursa hiyo kuwashukuru
watumishi wote wa wizara ya madini na taasisi zake kwa kufanya kazi kwa
pamoja kama familia moja na hivyo kuwezesha kupatikana kwa mafanikio
makubwa katika sekta ya madini.
‘’ Kuna wakati niliwaeleza kiu yangu ni kujengwa kwa taasisi imara. Nashukuru
hata wakati sipo kila taasisi iliendelea kufanya kazi zake vizuri. Kiu yangu ni
kuona wizara na taasisi zinafanya kazi kwa pamoja ili tuwatumikie watanzania
na tumalize matatizo ya wadau wetu.,’’ amesema Biteko.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amempongeza
Waziri Biteko kwa kuaminiwa na kuchaguliwa tena kuiongoza wizara ya madini
na hivyo kutumia fursa hiyo kumkaribisha tena wizara ya madini na kueleza ‘’
mafanikio yote yaliyopatikana ni yetu sote kwani sisi sote tulioongea lugha
moja,’’.
Comments
Post a Comment