Waziri wa Madini Doto Biteko amewashauri
Wadau wa Madini wa Mkoa wa Geita kuungana na kutengeneza Kampuni ya pamoja ili
kuongeza tija katika shughuli zao.
Ushauri huo, ameutoa mara baada ya
kutembelea Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini
yanayoendelea Mkoani Geita.
Wakati huo huo, Waziri Biteko ametoa
pongezi kwa waandaji wa Maonesho hayo ambayo mwaka huu zaidi ya kampuni 420 zinashiriki.
Waziri Biteko akisaini kitamu cha wageni katika banda la benki ya CRDB alipotembelea Maonyesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Septemba 21, 2020 mkoani Geita
Vilevile, Waziri Biteko ametoa Wito kwa
taasisi za Kibenki kuendelea kuwalea Wachimbaji Wadogo na Wafanyabiashara ya
Madini kwa kuwapa mafunzo pamoja na mikopo ili wazalishe kwa faida.
Naye, Mkurugenzi wa Mikopo kwa
Wajasiliamali Wadogo wa NBC Elibariki Masuke, amesema Benki ya NBC Mkoa wa
Geita imetoa mkopo wa zaidi ya Shilingi bilioni 4.4 kwa Wadau wa Sekta ya
Madini mkoani humo ili kuwaongezea uwezo katika shughuli zao.
Hayo aliyasema mbele ya Waziri Biteko
alipotembelea banda la la benki ya NBC katika Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na
Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Imeelezwa kuwa, wanufaika wa mikopo hiyo
ni pamoja na Wachimbaji Wadogo, Wafanyabiashara ya Madini na Wachenjuaji wa
Madini wa Mkoa wa Geita.
"Sisi kama Benki ya NBC tumeanza
kutoa mafunzo kwa Wadau wa Madini hususan Wachimbaji Wadogo wa dhahabu na
Wafanyabiashara ya dhahabu ili kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuwekeza
katika Sekta ya Madini", alisema Masuke.
Pamoja na mambo mengine, Masuke amesema Banki ya NBC imekuwa Mdau Mkubwa kwenye Sekta ya Madini ambapo mpaka sasa kuna taratibu zinawekwa sawa ili mikopo mikubwa zaidi ianze kutolewa kwa Wadau wa Sekta ya Madini kote nchini.
Comments
Post a Comment