Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaye shughulikia Uwekezaji Angera Kairuki leo Septemba 27, 2020 ameyafunga rasmi Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Mkoani Geita.
Aidha, Waziri Kairuki ameupongeza Mkoa wa Geita kwa maandalizi mazuri waliyoyafanya katika Maonesho hayo ambapo ametoa wito kwa mikoa mingine yenye madini kuiga mfano wa Geita.
Imeelezwa kuwa, Sekta ya Madini imekuwa kwa kiwango kikubwa ambapo mwaka 2015 ilikuwa ikichangia pato la taifa kwa asilimia 3.4 lakini kwa sasa mchango wake umepanda na kufikia asilimia 5.2.
Aidha, Waziri Kairuki, amewapongeza Wachimbaji Wadogo na Wafanyabiashara ya Madini kwa kulipa kodi kwa hiari na kufanya kazi zao kuwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Serikali.
"Serikali kupitia Tume ya Madini tumetoa zaidi ya leseni 801 kwa Wachimbaji Wadogo pia nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Madini kuwezesha kupata Cheti cha Ualisia kwa Madini ya Bati (Tin) ambapo wafanyabiashara wa madini hayo watayasafirisha na kuyapeleka kuuza mahali popotete Ulimwenguni"
Naye, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema Serikali imeendelea kutekeleza mipango ya kuwawezesha Wachimbaji Wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija na kuwaboreshea mazingira yao ya kazi pamoja na kuwatengea maeneo yenye taarifa za kijiolojia ili kiepusha kuchimba kwa kibahatisha.
Vile vile, Waziri Biteko ametoa wito kwa Wachimbaji Wadogo na Wafanyabiashara wa Madini kuyatumia maonesho hayo kama chachu ya kuwahimiza kutumia Teknolojia nafuu na zenye tija katika shughuli zao.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali akiwemo Waziri wa Madini Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt Philimone Sengate, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said.
Comments
Post a Comment