MAAFISA MADINI WAKAZI WA MIKOA WAMKOSHA WAZIRI WA MADINI

 
Waziri wa Madini,  Doto Biteko amewapongeza Maafisa Madini Wakazi  wa Mikoa kwa utendaji mzuri uliopelekea kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019-2020 ambapo walikusanya shilingi bilioni 528.2 ikiwa ni zaidi ya lengo la shilingi bilioni 470 lililopangwa awali.

Waziri Biteko ameyasema hayo leo tarehe 25 Julai, 2020 jijini Arusha alipokuwa akifunga mkutano wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa wenye lengo la kujadili mafanikio, changamoto na namna ya kuzitatua kwenye Sekta ya Madini.


Wageni wengine waliohudhuria katika mkutano huo ni pamoja na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Kamishna wa Madini Nchini, Mhandisi David Mulabwa, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Wakuu wa Idara na Mameneja kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Alisema siri ya mafanikio makubwa katika Wizara ya Madini ni pamoja na ubunifu na uzalendo wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwenye ukusanyaji wa maduhuli na kuwataka kuendelea kusimamia shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kwa kufuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.

"Nipende kueleza kuwa, ninatambua mchango wenu mkubwa sana kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini, mmekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kodi mbalimbali zinalipwa Serikalini, hii imesaidia sana Sekta ya Madini kukua.

Katika hatua nyingine Waziri Biteko amewataka Maafisa Madini Wakazi kutatua migogoro kwa kusimamia Sheria na kusisitiza kuwa wasisite kuwasilisha changamoto kwa viongozi wa Tume ya Madini pale wanapokwama.

Aidha, aliwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kushirikiana kwa kubadilishana uzoefu kwenye usimamizi wa shughuli za madini ili kuongeza tija kwenye utendaji kazi.

Naye Naibu Waziri Nyongo akizungumza kwenye mkutano huo, aliwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kushirikiana  kwa karibu na Wakuu wa Mikoa, Wilaya,  Taasisi nyingine pamoja na vyombo vya ulinzi na  usalama ili kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi wao.

Aliwataka kila mmoja kuhakikisha anatimiza lengo la makusanyo ya maduhuli kwa mwaka wa fedha 2020-2021 alilopangiwa ili Wizara iweze kuvuka  lengo la mwaka husika.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila mbali na kuwapongeza Maafisa Madini hao aliongeza kuwa, imani kwa Serikali kwa Wizara ya Madini imeongezeka mara baada ya kufanikiwa kukusanya maduhuli zaidi ya lengo lililowekwa awali.

"Mtakumbuka mwaka jana tulisaini mkataba wa shilingi bilioni 10.6 na Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuimarisha Tume ya Madini kwa kununua vifaa mbalimbali pamoja na magari ambapo zimezaa matunda, endeleeni kuchapa kazi na tupo tayari kuwasaidia muda wowote."alisema Profesa Msanjila.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula aliishukuru Wizara ya Madini kwa ushirikiano mzuri kwa Tume ya Madini hali iliyopelekea Tume kufanya vizuri kwenye Sekta ya Madini.

Alisema kuwa changamoto zilizoainishwa katika mkutano husika zitaandaliwa vyema na kuwasilishwa ngazi za juu na utekelezaji wake kufanyika mara moja.


Comments