Breaking: JPM ateua wengine, yumo Mkuu wa Mikoa, Wilaya, Makatibu Wakuu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Julai, 2020 amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali kama ifuatavyo ambapo amemteua Dr. Jumanne Fhika kuwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Njombe, kabla ya uteuzi huo Dr. Fhika alikuwa Ofisi ya Rais na anachukua nafasi ya Christopher Ole Sendeka.

Rais Magufuli pia amemteua Dr. Aloyce Nzuki kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, kabla ya uteuzi huo, Dr. Nzuki alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na anachukua nafasi ya Prof. Adolf Mkenda.

JPM pia amemteua Mhandisi Anthony Sanga kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Sanga alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na anachukua nafasi ya Prof. Kitila Alexander Mkumbo.

Wengine walioteuliwa ni Dr. Allan Kijazi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii akichukua nafasi ya Dr. Aloyce Nzuki aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, na pia Dkt. Allan Kijazi ataendelea kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Mhandisi Nadhifa Kemikimba ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi katika Wizara ya Maji na anachukua nafasi ya Mhandisi Anthony Sanga ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, mwingine aliyeteuliwa ni Fadhili Mohamed Juma kuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mkoani Geita.

Fadhili alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi na anachukua nafasi ya Josephat Paulo Maganga ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma akichukua nafasi ya Patrobas Katambi, Wateule wote wanatakiwa kuwepo Ikulu, Chamwino Dodoma tarehe 20 Julai, 2020 saa 4:00 asubuhi.

Comments