Biteko Asikitishwa Mgodi wa WDL Kutaka Kuuzwa Kinyemela


Waziri wa Madini Doto Biteko amesikitishwa na kitendo kilichotaka kufanywa na  Uongozi wa Mgodi wa Madini ya Almasi wa Williamson Diamond Limited (WDL), uliopo Mwadui Wilayani   Kishapu mkoa wa Shinyanga cha kutaka kuuza  Mgodi huo kinyemela  bila kuitaarifu  Serikali.

Hayo ameyasemwa leo Julai 5, 2020 na Waziri  Biteko alipofanya ziara  kwenye mgodi huo baada ya kuona matangazo ya kuuzwa kwa mgodi huo kwenye mitandao ya kijamii.




Waziri Biteko amesema  Serikali ina ubia wa asilimia 25 katika mgodi wa WDL, hivyo,  haiwezekani utake kuuzwa bila mbia wake kufahamu na kueleza kuwa,   kitendo hicho ni kukiuka taratbu na Sheria za nchi.

“Serikali ina ubia wa asilimia 25 kwenye mgodi huu kama mnataka kuuza mgodi lazima mtoe taarifa serikalini na mpate kibali, kwa mantiki hiyo serikali inapaswa kuwaadhibu kwa kutaka kuuza mgodi bila kibali huko ni kuhujumu nchi. Hvi mlituuliza serikali hatuna uwezo wa kununua mgodi na kuuendesha?,” amesisitiza  Waziri Biteko.



Kutokana na kitendo hicho, Waziri Biteko ameuagiza uongozi wa mgodi huo ifikapo Julai 10 mwaka huu  uwe  umetoa maelezo kwa maandishi kueleza sababu za kutaka kuuza mgodi huo bila mbia wake ambaye ni Serikali kujua na pia  kutoa taarifa ya kuwapunguza kazi wafanyakazi kisha kuwalipa nusu mshahara.

Amesema utaratibu uliotumika kupunguza wafanyakazi  kwa kutumia kigezo cha ugonjwa wa Corona  haufai na  Wizara ya Madini hawakubaliani nao kutokana na pia  wafanyakazi kulipwa mishahara nusu jambo ambalo linatoa wakati mgumu na kusababisha migogoro isiyo ya lazima.


Aidha, Waziri Biteko, amesema sababu ambazo  zinatolewa na  mgodi huo za kusitisha shughuli za uzalishaji na kutaka kuuza mgodi huo pamoja na kushuka kwa bei ya almasi duniani iliyosababishwa na ugonjwa wa corona, amezieleza kuwa hazina mashiko na kampuni husika inatakiwa kueleza  ukweli na  kama  imefilisika  ijulikane.

Waziri Biteko amesema sababu kubwa ambayo ingefanya mgodi huo kufungwa ni kushuka kwa uzalishaji na siyo uendeshaji, huku akihoji kama mgodi hauna fedha za kujiendesha ungetoa taarifa badala ya kuweka matangazo kwenye mitandao kuhusu kuuzwa mgodi wakati serikali haina taarifa.


Kwa upande wake,  Meneja Mkuu wa Mgodi huo Mhandisi Ayoub Mwenda, amekiri kuwa hawakutoa taarifa Serikalini juu ya kutaka kuuzwa kwa mgodi huo, huku akieleza kuwa walifunga mgodi huo April 8 mwaka huu kutokana na kushindwa kujiendesha na ameahidi kufuata maelekezo yote ambayo yametolewa na Waziri wa Madini.

Mhandisi Mwenda amesema Mgodi ilikuwa unazalisha vizuri kabla ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona ambapo kwa mchanga Iliyokuwa umezalishwa waliokuwa walikuwa mbele kwa asilimia tatu na almasi  zilizokuwa zimekusanywa  walikuwa mbele kwa asilimia 9.1kulingana na bajeti yao  Iliyokuwa  imewekwa

Amesema tatizo la Corona limeuathiri sana mgodi huo na kusimama kufanya shughuli za uzalishaji kutokana na kushuka bei ya masoko ya nje ambapo kabla ya Corona bei ilikuwa dola 246 kwa karati moja ambapo Machi mwaka huu waliuza karati moja dola 135 ambayo ilikuwa haiwezi kutosheleza gharama za uzalishaji.

Naye,  Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba ameipongeza Wizara ya Madini kwa kazi nzuri inazofanya  ambazo  zimeisaidia  nchi kuingia katika uchumi wa kati.

Comments