Saudi Arabia yapunguza idadi ya Mahujaji mwaka huu

Serikali ya Saudi Arabia imesema kuwa, kutokana na ugonjwa wa corona kuendelea kuzisumbua nchi mbalimbali duniani, itaruhusu idadi ndogo ya watu kutekeleza ibada ya Hijja mwaka huu.

Kila mwaka takribani mahujaji milioni mbili kutoka maeneo mbalimbali duniani wamekuwa wakifika Makka kwa ajili ya kutekeleza moja ya nguzo Tano za Kiislamu.

Saudi Arabia imesema uamuzi wake unalenga kuepusha maambukizi ya virusi vya corona ambavyo huenea kwa urahisi kwenye mikusanyiko ya watu.

Kwa mujibu wa Serikali ya Saudi Arabia, raia wa kigeni wanaoishi nchini humo wataruhusiwa kufanya Hijja kubwa ambayo inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.

Tangu mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu, ufalme wa Saudi Arabia ulisimamisha shughuli za Hijja ndogo yani Umrah kufuatia mlipuko wa virusi vya corona.

Comments