WAKAZI NYAMONGO WALIPWA FIDIA BILIONI 33/-


Waziri wa Madini, Doto Biteko akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa zoezi la ugawaji fidia kwa wananchi wa Vijiji vya Matongo na Nyabichune wilayani Tarime Mkoa wa Mara. (Picha na Wizara ya Madini).
Na Asteria Muhozya, WM

Bwawa la kuhifadhi Tope Sumu (TFS) katika Mgodi wa Barrick North Mara. (Picha na Wizara ya Madini).

HATIMAYE wakazi 1,639 wa vijiji vya Matongo na Nyabichune katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime Mkoa wa Mara wamelipwa fidia ya jumla ya shilingi Bilioni 33 baada ya kusubiri kwa kipindi cha miaka 10.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Azzan Zungu akizungumza jambo wakati wa zoezi la utoaji fidia kwa wananchi wa eneo la Nyamongo. (Picha na Wizara ya Madini).
Fidia hiyo imelipwa Mei 20, 2020 na Mgodi wa Barrick North Mara ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliyoyatoa wakati wa ziara yake mkoani humo ambapo alitaka suala hilo ikiwemo la uchafuzi wa mazingira yamalizwe haraka.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa utoaji fidia  na ugawaji wa cheki kwa wakazi hao waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ajili ya uendelezaji wa shughuli za mgodi huo, Waziri wa Madini, Doto Biteko amewahakikishia wote wenye haki ya kulipwa fidia hiyo kuwa watalipwa fedha zao.

Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima akizungumza jambo wakati wa utoaji wa fidia kwa wananchi wa vijiji vya Matongo na Nyabichune wilayani Tarime Mkoa wa Mara. (Picha na Wizara ya Madini).
Aidha, ametoa pongeza kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kueleza kuwa wizara hiyo ilifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha inamaliza mgogoro wa fidia uliokuwepo baina ya wananchi na mgodi huo.
Pia, amempongeza Mthamini Mkuu wa Serikali kwa kazi ya uthamini iliyofanyika hatimaye kuwezesha wananchi wanaopaswa kulipwa  fidia zao wanalipwa na kuongeza, “maisha ya kutegesha yamekwisha, Serikali haitakubali kushuhudia watengeneza migogoro wakitengeneza migogoro hapa”.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula, akizungumza jambo wakati wa utoaji fidia kwa wananchi wa vijiji vya Matongo na Nyabichune wilayani Tarime mkoa wa Mara. (Picha na Wizara ya Madini).
Katika hatua nyingine, ameiagiza Bodi ya Kampuni ya Twiga Corporation Limited kuhakikisha inaufungaminisha mgodi huo na shughuli za wananchi kiuchumi ili waweze kunufaika na uwepo wa mgodi wake.
“Tunataka Sekta ya Madini ifungamanishwe na sekta nyingine za kiuchumi, lakini ttunataka wananchi wa Nyamongo wafanane na dhahabu  inayochimbwa hapa,”amesisitiza Waziri Biteko.
Vilevile, ameutaka mgodi huo kuangalia na kuzifanyia kazi changamoto za kijamii zinazowakabili wananchi  wanaozunguka mgodi huo zikiwemo za maji, barabara na ili kujenga mahusiano mazuri na jamii hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Azzan Zungu amesema wizara yake imejiridhisha kuhusu usalama wa taka sumu na kuongeza kuwa mara kwa mara umekuwa ukifanyika  ukaguzi kuhakikisha maji hayo hayaathiri wananchi wanaozunguka mgodi huo. Pia, amewahakikishia wananchi kuhusu ufuatiliaji wa sheria na taratibu za mazingira kuhusu suala hilo.

Pichani ni wawakilishi wa wananchi wakipokea cheki za malipo ya fidia. (Picha na Wizara ya Madini).

Akizunguzia kuhusu matumizi ya zebaki, amewataka wachibaji nchini kuachana na matumizi ya zebaki kwani madhara yake ni makubwa pindi inapoingia mwilini.

Pichani ni wawakilishi wa wananchi wakipokea cheki za malipo ya fidia. (Picha na Wizara ya Madini).
Naye, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema zoezi la utoaji fidia lilichukua muda mrefu kwa sababu wananchi  hawakuwa wakitoa taarifa sahihi na baadhi kutegesha  na akatumia kutumia fursa hiyo kuwaasa wananchi  kutoa ushirikiano na kuwa  wa kweli kwenye masuala yote yanayohusu ulipaji fidia.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Migodi ya Barrick Hilaire Diarra,  amesema kampuni hiyo imeanza safari mpya ya amani, ufanisi wa pamoja kwa Maendeleo ya Jamii. Ameongeza kwamba, kwa miaka mingi mahusiano kati ya mgodi na jamii hiyo yamekuwa siyo mazuri lakini hivi sasa  mgodi huo unaamini katika kuyajenga upya.
Ameongeza kuwa, Kamati ya Maendeleo ya Jamii imeundwa ili kuangalia vipaumbele katika eneo hilo na yote yatafanyika kupitia kamati hiyo.
” Tumetembea miezi minne (4) kufikia hapa, makinikia, ushuru, utafiti, vibali vya kazi, wafanyakazi wa nje, Usajili wa Jina la Twiga. Nakumbuka mara mwisho Mheshimiwa Waziri ulikuwa bado ukisisitiza suala la fidia liwe historia,” amesema Diarra.
Wakizungumza katika mahojiano maalum, Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila amesema suala hilo lilichukua muda mrefu hatimaye sasa wananchi na mgodi wamekubaliana, hivyo kupelekea kulipwa kwa fidia hiyo ya shilingi bilioni 33.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo amesema wananchi waliofanyiwa uthamini wamepata fidia ya haki.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt.Samwel Gwamaka amesema,mamlaka hiyo inafanyia kazi malalamiko ya wananchi wanaozunguka migodi sambamba na kukagua iwapo taratibu za mazingira zinafuatwa.
Ameongeza kuwa, Barrick North Mara ni miongoni mwa migodi inayofuatiliwa kuhakikisha uendeshaji wake hauleti madhara kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Wateja wa Benki ya Benki ya CRDB, Boma Raballa, ameahidi kutoa huduma bora za kibenki kwa wananchi waliolipwa fidia kwa kuhakikisha inatoa elimu kuhusu matumizi bora ya fedha walizozipata ikiwemo kuhakikisha wanapata fedha hizo haraka.
Aidha, mbali na kushuhudia ufunguzi wa utoaji fidia,viongozi walioshiriki katika zoezi hilo pia wametembelea na kukagua Bwawa la Kuhifadhi Tope Sumu ( TFS) katika mgodi huo.

Comments