MAGUFULI -CORONA ISIWE CHANZO CHA KUTOELEWANA SISI NA KENYA



Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema Corona haikuanzia Afrika hivyo haipaswi kuwa chanzo cha kutoelewana kati ya nchi za Kenya na Tanzania, na kwamba nchi zote zinahitaji biashara.
''Huu ni wakati wa kujenga uchumi, Corona haikuanzia Afrika hivyo tusije tukachonganishwa sisi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tukashindwa kufanya biashara kwa kisingizio cha ugonjwa huu', amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alikua ziarani katika Mkoa wa Singida nchini humo.
Amesema amezungumza na Rais Uhuru Kenyatta juu ya njia za kutatua mzozo ulioibuka kwenye mpaka baina ya Tanzania na Kenya baada ya Kenya Kufunga mipaka yake ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona: ''Tumekubaliana na Rais Kenyatta kuwa Mawaziri wetu wa Uchukuzi pamoja na baadhi ya Wakuu wa Mikoa watakutana na wenzao wa Kenya kujadili kuhusu migogoro inayojitokeza mipakani '' amesema Rais Magufuli.
Amewataka viongozi wa pande zote mbili waweke maslahi ya Tanzania na Kenya mbele, waache kuamua mambo ya mpakani kwa jazba na ameagiza Wakuu wa Mikoa ya Mara, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert Ibuge kuhakikisha mazungumzo hayo yanafanyika ndani ya wiki moja.
Kauli hizi za rais wa Tanzania zinakuja baada ya Tanzania kujibu hatua ya Kenya kufunga mipaka yake na Tanzania ambapo ilizuwia malori kutoka Kenya kuingia nchini humo huku afisa mwingine wa ngazi ya juu akiwalaumu madereva wa lori wa Kenya kwa kuingiza virus Tanzania.

Rais MagufuliHaki miliki ya pichaMSEMAJI MKUU WA SERIKALI /TWITTER

''Virusi vya Corona vimepungua sana lakini havijaisha hivyo, tuendelee kuchukua tahadhari zote ambazo tunaelekezwa na wataalamu wetu. Singida kuna wagonjwa watatu tu mpaka sasa ambao wanaendelea vizuri'', ameongeza Bwana Magufuli.
Aidha amesema kuwa Tanzania sasa inaenda mbele '' Ipo katika nchi tano za Afrika ambazo uchumi wake unaenda juu na hivyo tunaendelea na miradi mbalimbali ya kimkakati ya kuitengeneza nchi yetu iwe kama ulaya'', amesema Magufuli.
Siku chache zilizopita umeibuka mgogoro katika vituo vya mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mikoa ya Mara, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro baada ya malori ya mizigo ya kutoka Tanzania kuzuiwa kuingia Kenya kwa madai ya madereva wanaopimwa kukutwa na ugonjwa wa Corona.
Wakati huo huo Taarifa ya viongozi wa Tanzania John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta imesema kuwa wamewaagiza Mawaziri wa Uchukuzi na Wakuu wa Mikoa iliyopo katika pande zote za mpaka wa Tanzania na Kenya kukutana na kutatua mgogoro uliosababisha kuzuiwa kwa malori ya mizigo kuvuka mpaka huo.
wamekubalina kuwa viongozi wa pande zote mbili wanapaswa kukutana na kuutatua mgogoro huo haraka iwezekanavyo ili Watanzania na Wakenya waendelee kufanya biashara zao kama kawaida, na kwamba kuzuiwa kwa malori ya Tanzania yanayokwenda Kenya ama kuzuiwa kwa malori ya Kenya kuja Tanzania hakukubaliki

Comments