MADIWANI WATOA MOTISHA KWA SHULE ILIYOFAYA VIZURI BUKOMBE









Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wametoa motisha ya vitambaa vya kushona suti kwa walimu na wajumbe wa kamati ya shule ya msingi Uyovu iliyo faulisha wanafunzi watatu bora wa shule za serikali kitaifa.

Akizungumza katika baraza hilo Afisa Elimu Taaluma shule za msingi Wilaya ya Bukombe Kassim Mussa alisema shule ya msingi Uyovu ni miongoni mwa shule za msingi za serikali 86 Wilayani Bukombe.

Mussa alitoa wito kwa walimu na viongozi wa kamati za shule kuendelea kufanya vizuri kwa kusimamia mikakati waliojiwekea.

Nae Afisa Elimu shule za msingi Wilaya ya Bukombe Shadurack Kabanga alisema katika ufaulu wa mwaka 2018/19 shule ya msingi Uyovu ilifanya vizuri kitaifa kutokana na hali hiyo halmashauri imetoa motisha kwa walimu na kamati ya shule.

Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya shule msingi Uyovu Emmanuel Mpandiko alisema wamekuwa na ushirikiano mzuri na walimu hali ambayo imewafanya walimu kuwa na hari ya kujituma katika ufundishaji .

 Mkuu wa shule ya msingi Uyovu Sevelin Jegu alisema nafasi walioshika mwaka 2019 ni haki yao kwani wamekuwa wakiweka kambi kila unapo karibia mtihani wa taifa na kuongeza kuwa mwaka huu wanamikakati waliojiwekea ili kuhakikisha wanafanya vizuri tena.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe na Diwani wa Kata ya Bulega Erick Kagoma aliwapongeza walimu wa shule ya msingi Uyovu na kuishukuru idara ya Elimu Wilaya kwa kutoa motisha kwa walimu walioiheshimisha halmashauri.

Comments