WIZARA YA MIFUGO YAPANDIKIZA NG’OMBE ELFU 38


 Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk Felix Nandonde akipandikiza mbegu bora ya ng'ombe   katika uzinduzi 

 Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk Asimwe Rwiguza akipandikiza mbegu bora ya ng'ombe   katika uzinduzi  


 Mfugaji wa Kijiji cha Kazibizyo Ibrahimu Ntugwa akimwangalia ng'ombe wake baada ya kupandikizwa mbegu bora.

Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk Felix Nandonde alisema mpaka sasa wamesha pandikiza ng’ombe Elfu 38  na Wizara kupitia bajeti ya mwaka 2020/21 imetenga Tsh milioni 167 kwa ajili ya kuhamasisha wafugaji kupata mbegu bora bure 

Dk Nandonde  aliyasema hayo wakati akizindua zoezi la   Uhimilishaji (Upandishaji wa mbegu bora za Ng’ombe uliofanyika katika Kijiji cha Kazibizyo kata ya Ng’anzo  kwa ng’ombe 86. 

Alisema  Tanzania kuna jumla ya ng’ombe  milioni 32.5 na zoezi hilo lilianza  Julai mwaka 2019 likiwa limelenga kuifikia mikoa 14 na kusisitiza kuwa Wizara imelichukua kama zoezi endelevu .

 Dk Nandonde  alisema  malengo ya Wizara ni kupandikiza ng’ombe milioni 3 nchi nzima ili kupata ng’ombe bora (chotara)  milioni 1  wenye uwezo wa kukua kwa haraka hali ambayo itawafanya wafugaji kukuza uchumi wa familia na taifa kupitia viwanda vya kuchakata nyama ngozi na kusindika maziwa hapa nchini.

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk Asimwe Rwiguza alitoa wito kwa wafugaji kutunza mifugo yao kwa kuiwekea mazingira bora ya malisho. 

Dk Rwiguza alisema Wizara imetenga maeneo ya malisho  milioni 2.8 kupitia matumizi bora ya ardhi  kuanzia ngazi za vijiji na Kata na kuziomba kila halmashauri kuendelea kutenga maeneo ya malisho kwa wafugaji ili serikali ifikie malengo katika mkakati wa Wizara. 

Kaimu Afisa Mifugo na Uvuvi  Wilaya ya Bukombe Asifiwe Mjujulu aliishukuru Wizara kwa kuwaletea  dozi 500 ya mbegu kwa ajili ya wafugaji ambayo itasaidia kuepukana na  ugonjwa wa (Bluselosisi) ambao unasababisha kutoka kwa mimba,  unaosababishwa na madume ya ng’ombe.

Kwa upande wake Mfugaji wa Kijiji cha Kazibizyo Ibrahimu Ntugwa aliishukuru serikali kwa kuwalete mbegu bora ambazo zitawainua kiuchumi mara tu watakapoanza uvunaji wa mifugo inayotokana na uboreshaji huo.

Comments