TRA yavunja rekodi ya ukusanyaji mapato Septemba 2019 trilion 1.7

Ni Headlines za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambapo Septemba 2019 imekusanya mapato ya Serikali jumla ya TZS 1.767 trilioni,makusanyo haya ambayo ni sawa na ufanisi wa 97.20% ya lengo  la kukusanya jumla ya kiasi cha TZS 1.817 trilioni katika kipindi cha mwezi Septemba 2019.
Aidha TRA wanasema hawajawahi  kukusanya mapato hayo ndani ya mwezi tangu kuanzishwa kwa TRA. Kwa kulinganisha na makusanyo ya mwezi Septemba 2018, makusanyo haya ya mwezi Septemba 2019 yamekua kwa wastani wa 29.18%.
Ufanisi huu wa mwezi Septemba 2019 ni mwendelezo wa ongezeko la makusanyo tangu mwaka wa fedha wa 2019/2020 ulipoaza mnamo mwezi Julai 2019. Hii ni kwa sababu katika kipindi cha mwezi Julai na Agosti 2019, TRA walifanikiwa kukusanya kiasi cha TZS 1.256 trilioni (ambayo ilikuwa ni ufanisi wa 91.92% ya lengo la kukusanya TZS 1.367 trilioni) na TZS 1.335 trilioni (sawa na ufanisi wa 96.05% ya lengo la kukusanya TZS 1.409 trilioni), sawia.
Aidha, makusanyo haya ni kiashiria kwamba Walipakodi na Watanzania walio wengi sasa wameelewa, wamekubali, na wameitikia wito wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.
Hivyo, TRA inawashukuru walipakodi wote waliochangia makusanyo hayo kwa kulipa kodi zao kwa hiari. Pia, wanaishukuru Serikali (kwa ujumla wake) kwa kuendelea kuisaidia TRA katika kutekeleza majukumu yake ya kukusanya na kuhasibu mapato ya Serikali.

Comments