Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 30 Septemba, 2019 amepokea taarifa ya utekelezaji wa ushauri alioutoa tarehe 22 Septemba, 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 30 Septemba, 2019 amepokea taarifa ya utekelezaji wa ushauri alioutoa tarehe 22 Septemba, 2019 kuhusu kuwasamehe washtakiwa wa makosa ya uhujumu walio tayari kukiri makosa yao, kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali.
Akitoa taarifa hiyo Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga amesema kwa kipindi cha siku 7 zilizotolewa, washtakiwa 467 wameandika barua na kuomba kurudisha jumla shilingi Bilioni 107 na Milioni 842.
DPP Mganga amefafanua kuwa kati ya fedha hizo wapo washtakiwa waliotayari kulipa hivi sasa kiasi cha shilingi Bilioni 13 na Milioni 602 pamoja kukabidhi Serikalini madini yakiwemo dhahabu na Tanzanite yenye jumla ya kilo 35, na pia wapo washtakiwa waliotayari kulipa shilingi Bilioni 94 na Milioni 240 kwa awamu.
Ameongeza kuwa pamoja na fedha hizo, wapo washtakiwa wengine wawili walioitikia zoezi hili na hivyo kukiri makosa yao Mahakamani ambapo mmoja wao amelipa shilingi Bilioni 1 na Milioni 37 na amekabidhi Serikalini gramu 2,123.64 za madini ya vito yenye thamani ya shilingi Milioni 36.5.
Aidha, DPP Mganga amemuomba Mhe. Rais Magufuli aongeze siku kwa watuhumiwa kuwasilisha barua zao za kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali kutokana na baadhi yao kushindwa kufanya hivyo kwa kipindi kifupi cha siku 7 kutokana na sababu mbalimbali.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza DPP Mganga na timu yake kwa kazi nzuri waliyofanya katika utekelezaji wa ushauri huo na pia kwa namna wanavyoiwakilisha vizuri Serikali katika kesi mbalimbali Mahakamani.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na mwitikio wa washtakiwa wengi kujitokeza kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali wanazodaiwa kuhujumu, na ameagiza washtakiwa wote waliofanya hivyo waanze kuachiwa kutoka Magerezani waliokokuwa wanashikiliwa.
Amekubali kuongeza siku 7 kwa DPP kuendelea kupokea barua za washtakiwa ambao wapo tayari kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali na ameonya kuwa baada ya muda huo hakutakuwa na msamaha mwingine na kwamba kutolewa kwa msamaha huo hakuna maana kuwa makosa ya uhujumu uchumi yamefutwa.
“Nafahamu wapo wengine wanadanganywa na Mawakili wao kuwa wakikubali ndio watakuwa wamejifunga, hapana, wakisamehewa wamesamehewa, lakini sio lazima kuomba msamaha wakitaka kuendelea kubaki Magerezani ni shauri yao.
Lakini wale ambao wameomba msamaha na wamelipa waachieni hata leo, na wasirudie tena kufanya makosa hayo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Magereza na Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na Ofisi ya DPP katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Amebainisha kuwa fedha zitakazokusanywa kutoka kwa washtakiwa hao zitalinufaisha Taifa kwa kwenda kutumika katika maendeleo ya wananchi ikiwemo ujenzi wa hospitali na barabara na kwamba ni matarajio yake kuwa washtakiwa watakaoachiwa watakwenda kushiriki ujenzi wa Taifa kwa njia zilizo halali.

BONYEZA HAPA CHINI KUTAZAMA VIDEO

Comments